Wabunge wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala), jana walimng’oa madarakani Spika, Dk Margret Zziwa baada ya kukubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Sheria, Kanuni na Madaraka ya Bunge kuwa amepoteza sifa za kuendelea kushikilia wadhifa huo.
Wabunge 36 kati ya 39 waliohudhuria kikao cha dharura cha Bunge hilo kilichofanyika hapa jana chini ya uenyekiti wa Kaimu Spika, Chris Opoka-Okumu walipiga kura za ndiyo kukubali hoja hiyo.
Wabunge wawili walipiga kura ya hapana, wakati mmoja hakupigia kura hoja hiyo iliyowasilishwa na mbunge wa Kenya, Peter Mathuki Machi mwaka huu na kuibua mvutano miongoni mwa wabunge waliokuwa wakimtetea Zziwa na wale waliotaka ang’oke.
Uamuzi wa kumng’oa Spika umechukuliwa kwa kuzingatia Kifungu cha 53(3) cha katiba ya kuanzishwa kwa EAC, inayowapa mamlaka wabunge kumwondoa ofisini Spika.
Mwenyekiti wa kamati uchunguzi dhidi ya Spika Zziwa, Frederick Ngenzebuhoro kutoka Burundi alisema madai yote dhidi ya kiongozi huyo yamethibitika kuwa kweli na kuomba Bunge lipitishe azimio la kumng’oa madarakani.
“Baada ya kuchunguza, kufanya mahojiano na kukusanya nyaraka mbalimbali zikiwamo barua za Spika Zziwa mwenyewe, picha za mgando na video, kamati inapendekeza aondolewe madarakani mara moja kwa kushindwa kutimiza wajibu na matumizi mabaya ya madaraka,” alisema Ngenzebuhoro katika taarifa yake ya kurasa 18 kuthibitisha tuhuma dhidi ya Dk Zziwa.
Awali, kabla ya uamuzi huo, Mwanasheria wa Spika Zziwa, Jet-John Tumwebaze alizungumza na waandishi wa habari na kudai kuwa kikao cha Bunge cha jana ni batili kwa sababu hakiko kwenye kalenda na kinaongozwa na Kaimu Spika, cheo alichosema hakipo kikatiba.
Alisema kamati iliyochunguza tuhuma dhidi ya Dk Zziwa haikuwa huru kwa sababu wajumbe 11, kati 15 ni miongoni mwa waliosaini hati ya hoja ya kumng’oa madarakani.
Mtoa hoja Mathuki alielezea furaha yake baada ya Bunge kupitisha azimio la kumwondoa madarakani kiongozi huyo.
“Nimefarijika kuwa Bunge hili limethibitisha pasipo shaka kuwa hoja yangu ililenga masilahi mapana ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na siyo ajenda binafsi kama baadhi walivyojaribu kupotosha,” alisema Mathuki.
Kwa uamuzi huo, Uganda inapewa fursa ya kuteua mtu au watu watakaopigiwa kura kushika wadhifa huo kwa sababu kiti hicho kinashikiliwa kwa kupokezana miongoni mwa nchi wanachama na hii ni zamu ya Uganda. Katibu wa Bunge, Kenneth Madette anatakiwa kutumia Kifungu cha 7(3), cha kanuni za Bunge hilo, kutangaza kuwa nafasi ya Spika iko wazi na kutoa fomu za kugombea kwa wabunge wanaotaka kuwania nafasi hiyo ndani ya saa 48 tangu kiti kinapobaki wazi.
Tuhuma
Spika Zziwa anadaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kuwaingiza baadhi ya ndugu zake akiwamo mumewe kwenye shughuli za Eala wakati siyo wabunge wala watumishi wa Bunge hilo.
Anatuhumiwa kwa upendeleo na ubaguzi miongoni mwa wabunge pamoja na matumizi ya lugha na kauli za kudhalilisha dhidi ya wabunge na watumishi wa Eala.
via>>Mwananchi
0 maoni:
Post a Comment