Fani ya Hip Hop kama wengi sasa hivi tujuavyo imejengwa na mihimili ama kanuni kuu nne, na ya tano ambayo ilianza kutajwa baadae:
- Udijei
- Mabreka
- Michano
- Machatta
- Ufahamu
Kanuni ya ufahamu ilikuwepo ila haikuwa ikitajwa, na inatokana na kuwa inagusa hizo kanuni nyingine nne zote. Baadae ikaanza kutajwa kama kanuni inayojitegemea.
Kati ya kanuni hizo kipengele cha michano ndicho kinachovuma sana hadi sasa na kufanya hata baadhi
ya watu kufikiri kuchana ndio Hip Hop. Kiukweli michano ni michano lakini sio kila anayechana ni MC au emcee (emsii). Kama Stic Man wa Dead Prez anavyosema, “Ni kama vile kuwe na mpiganaji wa mapigano ya kitaa na mtu aliyefunzwa na kufuzu sanaa ya mapigano.”
Kawaida mpiganaji wa mtaani ni mpiganaji, lakini huyu aliyefuzu na mfanyaji mazoezi ya sanaa ya mapigano anakuwa na uwezo wa ziada. Huu mfano ndio tofauti kubwa iliyopo kati ya mchanaji wa kawaida na MC.
Kuna mambo mengi yanayohusika mtu kuitwa MC. Moja wapo la msingi ni umahiri wa ushairi, anavyomudu lugha na uhodari wa kutamba tenzi au michano. Ule umahiri unakupa fursa ya kuwa pamoja na mdundo. Naelewa kwa nini kuna mijadala mingi sana inayohusisha tofauti ya mghaniji wa kawaida na MC.
Nataka kutumia mfano wa mtu ambaye ananijia upesi, ni Biggie Smalls au B.I.G. Biggie ni moja ya wale MCs ambao ukiwaangalia kijuujuu unaweza kudhani kuwa ni wachanaji ambao hawana ujumbe, wanajisifu tu; kumbe ujumbe upo ila ule utamu wa mashairi ndio kauweka mbele. Kuhusu uchanaji wa Biggie, nimewahi kusikia watangazaji, hata wa Marekani (Weusi), wakisema kuwa jamaa hasemi lolote, hayo yote ni maoni yanayotokana na kutazama juu juu.
Biggie alizipa kipaumbele mbinu za kutunga na yeye binafsi akawa anaburudika kutambaa mashairi yake, huku ujumbe unanyunyiziwa mdogo mdogo ili isichoshe. Biggie ana uwezo wa ajabu sana wa kucheza na maneno, na ukisikiliza wimbo “Unbelievable” utaelewa ninachokisema. Jambo jingine ambalo ni la nadra sana ni kwamba Biggie alikuwa akitunga na kuandikia mashairi yake kichwani bila kuweka kwenye karatasi.
Ujumbe dhidi ya ufundi
Suala la msisitizo wa ujumbe pekee, bila kuzingatia ufundi wa ushairi na mbinu za mitambao, ndio limedumaza watu wengi na kupoteza ufahamu wa watu kuhusu maudhui ya Hip Hop. Hilo ndio msingi uliovunjika na kupelekea hali iliyopo kwenye mtazamo wa ushairi wa Hip Hop; Bongo watu wamefanywa wasilijue kutokana na msisitizo mkubwa wa vyombo vya habari.
Msisitizo wa ujumbe umekuwa mkubwa mno lakini ukiangalia kiundani suala wanaoongelea sio ujumbe bali ni “mahubiri”. Nasema hilo kwa vile ujumbe ni ule uwasilisho, inaweza kuwa jambo lolote, kushindwa kwa mpokeaji kupokea sio kutokuwepo kwa ujumbe. Hilo nalo likaleta athari ya watu kuona kuwa kuchana ni “mahubiri yenye vina”.
Kama mpenzi wa dhati wa fani hii basi unaweza kuelewa ninachoongelea. Hali hii ilianza kujitokeza nyakati za kipindi cha DJ Show cha Radio One, miaka ya 95-96. Japo DJ Show ilifanya kazi nzuri ya kutoa fursa, lakini pia inahusishwa na kudhoofisha Hip Hop halisia, pengine si kwa makusudi. Kipindi hicho mahiri kilikuwa chini ya uasisi wa Taji Liundi au Master T, na baadae Mike Mhagama
Kwa mfano, majina yaliyotajwa na Mike Mhagama hapa hayahusiani na uwepo na muda. Alichanganya Fresh-XE na Kwanza Unit, ambao wanapishana miaka mitatu au zaidi. Akaweka Rhymson na kina Sugu na Swaleh Jabir, wanaopishana miaka mitano; yeye hakuwa anashughulikia mlolongo wa muda hapo.
Mashindano ya Michano
Kwenye miaka ya 88/89 kulikuwa na mashindano mengi ya mabreka, udijei na baadae mashindano ya kucheza disko — chini ya Maumba na Lundenga (huyu wa miss Tanzania). Kulikuwepo mashindano ya michano Kimara Studio 2000 Discotheque, chini ya DJ Mac Japhet, ambaye pia alikuwa anachana, kule Kimara Safari Resort.
Vikundi na watu wengine walioshiriki ni kama Villain Gangstar, Hard Core Criminal, Rankim Ramadhani na wengineo. Kwenye mashindano michano ya Lang’ata, mwaka 88, ushindi akapewa Dika Sharp.
Msisimko mkubwa wa mashindano ya michano uliimarika mwaka 91/92 — kulikuja mashindano ya michano yaliyoitwa Yo! Rap Bonanza. Jina hilo lina uakisi wa kioo kikubwa cha Hip Hop cha zama za dhahabu (1990-1995 au miaka ya jirani na hapo); ni jina linaloshabihi kipindi cha runinga cha MTV kilichojulikana sana kama Yo MTV Raps (huko Marekani). Mashindano haya yaliandaliwa na marehemu Kim, ama Abdulhakim Magombelo (M.A.P.), ambaye alikuwa mwandaaji matamasha mashuhuri. Kulikuwa na changamoto kubwa. Kuna waandishi wa kigeni waliokuja na kuhoji pengine watu wasiokuwepo na kuchapa vitabu vyenye upotoshaji wa hali ya juu. Kwa mfano mwandishi Alex Perulo. Waraka huu una mapungufu na upotoshaji wa hali ya juu. Makala ya kusahihisha upotoshaji huo zipo njiani.
“AP: Hip Hop History in Tanzania[Hip Hop] goes back to 1984 actually. Fresh X and Conway Francis were able to get recordings from the United States and Europe. Before that, he was a socialist country, and it was very difficult to get any materials from outside the country, including VCRs, television sets, cassette recorders, and records. The only way to be able to get things was if you had family abroad. Well Fresh Z and Conway Francis both came from fairly well-off families. They live in Oyster Day, which is a well-to-do neighborhood of Dar es Salaam. So they were able to get recordings and watch videos like “Breakin’” Breakin’ 2-Electric Boogloo”.“
Kama huna ufahamu wa historia ya muziki wa kizazi kipya, hicho kipengele ukikutana nacho kwenye kitabu ni rahisi kukipokea na kukipa mamlaka yote. Jina Fresh XE (Edo Mtui) ni jina la msanii wa kweli lakini mwaka uliotajwa sio wa kweli (Fresh alikuwepo zaidi katika miaka ya 87-91). Ule mwaka (1984) ni wa mabreka, mashindano ambayo Fresh hakushiriki. Alivyorudia jina hilo mara ya pili akamuita “Fresh Z” — sawa, labda ni kosa la kimaandishi, lakini ukitaka kuona huu utafiti una utata ni pale anapoongelewa Conway Francis (alizaliwa kama Fikirini), na kusema ametoka kwenye maisha ya unafuu. Conny amezaliwa Mwanza na baadae kuhamia Dar na kukulia Ilala, mitaa ya Mwanza/Arusha. Kwenye hali ile ile ya mpela mpela ya kitaa Bongo. Hakuwa akinunua hizo santuri bali alizikuta pale Vision au New Space (Disco lililokuwa jirani na jengo la IPS, mtaa wa Samora Dar).
Conny ni moja ya watu waliofanya hata mimi nipate hamasa ya kuchana. Kwenye zama za picnics alikuwa akitokea na kukamata muanzi na maujiko yote yalikuwa yakimuangukia yeye. Yeye alikuwa DJ zaidi kuliko mchanaji, na kikubwa ambacho anakumbukwa ni kwamba, alikuwa na sauti nzuri sana, kubwa. Ila mashairi yake ambayo mengi ni ya kukariri, alianzia kuchombezea kwenye disco. Ilikuwa rahisi yeye kupata nafasi ya ala za kuchania, na alikuwa na kinasa muda wote kule disco.
Baadae wakaja kuunda kundi liitwalo Three Power Crew; yaani, Con-way Francis, Fresh XE na Young Millionear (Usungu wa RFA). Hilo sio la msingi, bali ni kidokezo muhimu.
Ninachotaka kuongelea ni kuwa, kwenye mashindano ya Yo! Rap Bonanza kuliweza kutokea msisimuko mkubwa sana kwenye Hip Hop ya Bongo, na ni hapo hapo pia ulitokea pia upotoshwaji mkubwa.
Kwenye mashindano haya ya Yo! Rap Bonanza, kama kawaida ya Bongo, kulikuwepo majaji ambao si wasikilizaji wala vichwa wa Hip Hop. Kwa hali hiyo vigezo vilivyotumiwa vilikuwa havihusiani na umahiri moja kwa moja wa mchanaji na ubora wake wa utenzi. Moja ya vigezo ambavyo wao walivikazia zaidi ni “ujumbe”; lakini ambacho kilikuwa kinaitwa ujumbe ni “mahubiri”. Hapo tayari kwenye kanuni za ushairi tukajikuta tunaanza kupotea.
“…in 1991, there was a competition called “Yo Rap Bonanza” at the New Africa Hotel in Dar es Salaam. This featured a lot of great musicians: Ningawan, Easy B, D-Robb, KBCY. All these famous Tanzanian artists. In 1991, all groups were performing in English. The big thing was to copy, word for word, the American songs. Using the same music and everything. But then one artist at that competition named Saleh Ajabry performed a song based on “Ice Ice Baby” by Vanilla Ice. But he wrote the lyrics in Swahili, and he wrote it partly about HIV and AIDS. This is 1991! This was a hit, the first single to be released! People were really excited about this. And he won the competition for “Yo Rap Bonanza”. So that’s really the start of this Swahili-oriented Rap, beginning with Saleh Ajabry. And then all these other rappers, hearing this album now being played on cassette all over Dar es Salaam, are picking up on the message. That’s really where it started, the Swahili part about it.“
Nimemnukuu huyo mwandishi hapo juu. Sitatafsiri kama ninavyofanya kawaida ila nia ni kuonesha upotoshaji dhahiri. Japokuwa jamaa amewezeshwa vizuri na Chuo Kikuu alichotoka, Bryant, na kujipatia uprofesa mwandamizi, aliandika taarifa ambazo hazikufanyiwa utafiti wa kina. Hapo sijagusia jinsi gani majina yalivyovurundwa.
Kutokana na uwezeshaji alioupata angeweza kuwapata wasanii wahusika ambao wengi walikuwa hai alipofika mwaka 98 ama miaka mingine. Badala yake, yeye alikusanya taarifa nyingi toka vyanzo visivyoaminika. Magazeti yana taarifa hizi, baadhi ya watu walikuwa maredioni — kama K-Singo alikuwepo nchini, Bony Luv alikuwepo Clouds FM (mikato ya Dr. Beat, nini!), Othman Njaidi na wengine wengi tu. Hawa wanaujua mchezo nje ndani. Sasa, kama mtu anataka kujua lolote kuhusu historia ya muziki wa kizazi kipya, kwa nini asiwatambue wahusika!? Hapo ndipo upotoshaji ulipoanza kuota mizizi.
Wimbo aliouzungumzia hapo juu ilikuwa sio ya kwanza kwa Kiswahili Bongo, bali ni ya kwanza kupewa umaarufu, na umaarufu huu ulitokana na kupelekwa kwenye mzunguko wa wauza kanda. Watu walishaanza kuchana Kiswahili tokea mwaka 89.
Kuna vikundi vilikuwepo International School of Tanganyika (IST) mwaka 91, tayari walikuwa wana nyimbo zao za Kiswahili. Hao walikuwa kina Cool X (Samia X), Cool Moe Cee (Mosi Kipokola) na jamaa mwingine kutoka Malawi, B-Soul (Yamikani), na kundi lao la RRR – Ruthless Rhymes Renegades. Hapo sijaongelea ule wimbo wa Dika Shap — japo haukuwa Hip Hop kihivyo — alipomuimba Rais Mwinyi, mwaka 88 kama sikosei, Lang’ata.
Kwenye moja ya mashindano Yo! Rap Bonanza (yalifanyika mwaka 1992, ghorofa ya saba New African Hotel), alipewa ushindi jamaa anaitwa Saleh Jabir, na wa pili alikuwa KBC ama K-Singo. Mimi binafsi nafikiri KBC ndio alifaa awe wa kwanza; hapo tayari KBC na baadhi ya watu wa KU wanachana toka mwaka 1988. Huyo mshindi (Saleh) mwaka huo huo miezi michache nyuma alikuwa ni mcheza shoo (sio mchanaji), na kwenye maonesho yetu Lang’ata (Kinondoni karibu na American Chips pale) alikuwa akiingia na kufanya shoo za uchezaji wa MC Hammer na Vanilla Ice na jamaa zake wa Ilala. Nimedokeza hilo ili upate mwanga kidogo kuhusu mchanaji na MC hapo.
Shindano lililofuatia walishinda Kwanza Unit. Hili la pili haliongelewi sana, lilifanyika Empress Cinema, jengo la pili kwenye kona ya sanamu la bismini (Mnara wa Askari), kulia kwenye mtaa wa Samora, mwaka 1993 (tunaweza kuhakiki miaka kama nimekosea hapo).
Nakumbuka hapa II-Proud (siku hizi Sugu, ambaye alitokea mkoani Mbeya) alileta kash kash kidogo kuona kama alionewa kwenye matokeo, ilifikia hadi watu karibu washikane lakini ikatulizwa getini. Nia yangu si kuweka hizo taarifa za kihistoria, bali ni kukujengea mandhari iliyofungamana na matukio yalioleta athari zilizopo leo. Watu wa vyombo vya habari wakaanza kuvutiwa na wingi wa watu na uchangamfu wa hayo mashindano. Na kwa uchache wa ufahamu wao wa fani ya Hip Hop, wakaanza kuandika wanachokijua. Na hakukuwa na juhudi sana za kutuhoji kuhusiana na mantiki mbali mbali za Hip Hop zaidi ya kukebehi kwamba jamaa wanaigiza “Umarekani”.
Michano ya ‘Kinyamwezi’
Kipindi hiki cha miaka kati ya 88 hadi 93 watu (wengi waliojumuika na kuunda Kwanza Unit) walikuwa wanashinda na kanda za nyimbo za Hip Hop za New York, na ni kawaida kichwa akajua nyimbo hata kumi zote za santuri moyoni. Na ni kipindi ambapo disco la Clouds pia lilikuwa linapata kila santuri na single kutoka Marekani.
Nyingi ya santuri zile zilikuwa kama hivi. Na Kwanza Unit (baadhi, kabla haijawa KU Crew) walikuwa mara nyingi wanashinda Mawingu, hata kabla hakujawa studio ya kurekodi. Vilinge hivi vilijumuisha uangaliaji wa video za muziki na filamu za Marekani, soultrain video, kanda za redio kama zile za Tim West Wood (DJ maarufu sana wa Hip Hop na mtangazaji wa redio), n.k. Hizi kanda watu wanazo hadi leo.
Uwezo wa kuchana wa hawa watu wa karibu ulikuwa mkubwa kiasi kwamba kama wanachana nyimbo ya mtu inafanyika kama ambavyo unaisikia kwenye CD leo na zao za kuandika. Japo chache zilikuwa zimeathiriwa na mitambao ile asilia ya New York ama si’ ndio?
Hili jambo lilikuwa linaleta kero kwa baadhi ya watu hasa ukizingatia Bongo kuna zile za kuzimia sana Unyamwezi. Na kama mtu akiwa anaweza Kinyamwezi na anachukulia poa basi kuna aina ya chuki ikawa tayari imejengwa dhidi ya watu wa kundi hilo. Kabla hata ya kuwa K.U., msemo maarufu ulikuwa ni ‘hao mabishoo wa aistii (IST), wanajitia Wanyamwezi sana hao, ushaona enh!?’
Ni mambo ya kawaida ya vijana, maana baadhi yetu wengi hatukusoma shule ile, ila ilikuwa tu utundu wa kitaa uliofanya kuongea Kinyamwezi kuwa sio kesi, jambo ambalo lilirahisisha sana msingi wa mitambao. Hiyo dhana potofu ya kwamba watu wanaigiza Umarekani ndio lilifanya hata wale kina Perullo na wenzao wakija waambiwe kuwa ‘hao jamaa wanajifanya Wanyamwezi kwa sana’. Mtu yeyote aliyepata nafasi ya kusikiliza santuri ya mwanzo ya Kwanza Unit anapata picha tofauti, watu walikuwa tayari wana mwamko wa Umajumui Afrika na mfumo wao tayari wa kifalsafa Kiswa-centric.
Vilinge
Vilinge mahususi vilianzishwa wakati wa disco siku za Ijumaa New African Hotel, baada ya kufungwa kwa disco la Motel Agip (palikuwa panaitwa ‘Shimoni’), bila kusahau disco la Twiga (Mtaa wa Samora). Bonny Luv alikuwa akisimamisha disco kwa kama dakika 20 hivi na kumwachia K-Singo achane; miaka ya 89-90 au jirani ya hapo. Bonny alikuwa anamfahamu KBC na anaujua uwezo wake. Baada ya hapo wakajitokeza kundi la Riders Posse (Nigga One, James Wamba, DJ Wiz). Wiz alikuwa mbaya sana wa midundo-kinywa (beatbox), mtindo ambao leo watu hawafanyi kabisa Bongo. Hili ndio kundi ambalo waliungana na KBC na kuwa wamoja kama Raiders Posse.
Umahiri wa Michano
Kwa vile nimeshadokeza mtiririko wa kihistoria, natumai wanaotaka mnaweza kutafiti zaidi na kupanua huo mjadala ili historia ya fani iimarike zaidi. Narejea kwenye ufundi na umahiri wa michano ambayo ndio mada yetu ya leo.
Kuchana kuna vipengele muhimu kama;
Miundo-vina
- Mitambao — mitambao inajengwa na mistari yenye vina.
- Vina ni maneno yenye silabi zinazoshabihiana mbili au tatu za mwisho kwenye tenzi (shairi). Msisitizo ni sauti na zinavyosikika na sio zinavyoonekana kimaandishi. Kwa lugha ya kigeni vina wanaita ‘rhymes’ (inahusika na Rhymson, Mwana’vina, jina langu la zamani).
Kwenye kamusi ya Webster wanatafsiri “vina” namna hii:
(a) correspondence in terminal sounds of units of composition or utterance (as two or more words or lines of verse).(b) one of two or more words thus corresponding in sound(c) correspondence of other than terminal word sounds: as (1) alliteration (2) internal rhyme
(a) mashabihiano ya sauti za mwisho za vipande vya matamshi (kama maneno mawili au mistari ya beti).(b) neno moja ama mawili yanayoshabihiana kisauti(c) mshabihiano mwengine zaidi ya maneno ya mwisho wa (1) alliteration vina vya ndani vya mrejeo (sina neno la Kiswahili kwa sasa) (2) vina vya ndani (hivi ni maarufu sana kwenye mashairi ya Kiswahili).
Nia ya kuweka mifano hiyo si kwamba hizo tafsiri za lugha ya kigeni ndio mwongozo wetu, ila ni kuonesha kwamba kanuni za ushairi zipo wazi. Na kama kusingekuwa na tatizo la vina kwa MCs wa zama hizi Bongo, nisingeandika hii makala. Kwenye hali ya kawaida, MC au mchanaji wa kweli haya anayajua moyoni bila kupitia kitabu. Imenibidi nitafute namna nyepesi na ya kitaalamu kufahamisha wale wenye tatizo, wale nyota wanaobisha kuelekezwa wakiwa studioni (majina tunayahifadhi… kwa sasa), na wasanii chipukizi wanaotaka kujua na wanaathiriwa na wanachokisikia redioni, na kutukuzwa kama ni kazi bora.
Nakaribisha huu mjadala na nina ushahidi wa wachanaji kadhaa, ambao ni nyota, walioacha kufanya kazi, na muandaaji mahiri aliyeishi maisha yake yote anachana na kunyonga midundo, Lindu (Big One Production), ambaye kwangu naona ni hazina kubwa iliyotelekezwa Bongo. Yeye alikumbwa na tatizo la kutoelewa kwanini MCs wananuna wakielekezwa, hasa na mtu ambaye ana uzoefu na umahiri wa miaka yote nyumbani na mbele. Hii ni miaka ya 2000 – 2002 wakati aliporejea nchini toka Australia, alipokuwa akisoma na kuishi kwa miaka mingi.
Hali hii tete imepelekewa na hulka ya wasanii wa Bongo ya kutokubali kukosolewa na kuelekezwa, kigezo chao kikubwa ni kuwa kama ningekuwa sijui mbona redio inapiga kazi zangu (Je, kwa vichocheo gani? Mbona nafanya shoo ya watu 5,000, wewe hapa na kistudio chako hiki hakuna anayekujua utanambiaje hivyo?). Ni kwa hulka hii ndio maana fani ya Hip Hop inapitwa na manufaa mengi. Wenye ujuzi wamekaa hawatumiwi, na wasio nao wale wa kuunga-unga wanapewa nafasi kupitiliza. Na waliojinyakulia mamlaka ya kuwakilisha ni watu wasio wapenzi wa fani, wanafuata mkumbo kwa vile msukumo wa Hip Hop haustahimiliki.
Najua hii mada italeta mjadala mkubwa nami naukaribisha hapa kwa moyo mkunjufu, hadharani na hata anayetaka kuufanya faragha.
Mitambao kwenye uchanaji unategemea na:
- Mianguko ya kifundi sana juu mdundo ambayo huwa inakaa sambamba ndani ya hesabu ya nne-nne. Hizo hesabu ndio kutoka mkito kwenda mlio wa snea (snare). Kawaida mstari huwa na urefu wa mkito hadi snea.
- Kasi ya mchanaji
- Mirindimo inayoingiliana, na jumla ya yote hayo juu
- Mtiririko na wa kupanda na kushuka kwa sauti
- Lafudhi; inayohusisha rhythm na enunciation (utamkaji)
Hiyo mianguko inajulikana kigeni kama ‘cadence’:
1. (a) a rhythmic sequence or flow of sounds in language (b) the beat, time, or measure of rhythmical motion or activity2. (a) a falling inflection of the voice (b) a concluding and usually falling strain; specifically : a musical chord sequence moving to a harmonic close or point of rest and giving the sense of harmonic completion3. the modulated and rhythmic recurrence of a sound especially in nature
Sitopenda kuingia ndani sana humu kwenye hesabu na fizikia ya michano hadi tutapoanza somo la vina rasmi. Natumai kwa mtiririko wa makala hii nimeweza kugusa maeneo yote muhimu. Na ndugu msomaji, kwa mchanganyo wa historia na vielelezo vichache hivyo, unaweza kupata mwanga wa jukumu alilonalo msanii hadi aitwe Manju Chenguzi, MC au emsii. Kwa heshima, taadhima na kwa ridhaa yenu naishia hapo.
Tuko pamoja!
Zavara Mponjika Mtigino.
Mwandishi, Mchambuzi wa Sanaa na Utamaduni
Mratibu Sanaa, Mtengeneza filamu, Muasisi wa Sanaa
Msomi Mwalikwa Chuo Kikuu cha Yale, Marekani
Barua pepe: zavara (at) tzhiphop (dot) com
0 maoni:
Post a Comment