WANA HABARI KUTOKA TANZANIA WAFUNGUKA MENGI KUHUSU ZIARA YAO NCHINI GHAN
Na Yohana Emmanuel-Accra Ghana
Ziara ya Mafunzo ya waandishi na viongozi wa vyombo tisa vya habari kutoka Tanzania nchini Ghana, imekuwa ya mafanikio makubwa kufuatia timu hiyo kujionea mambo mbalimbali ya muhimu katika uboreshaji wa sekta ya habari nchini Tanzania.
Meneja wa Radio Kahama FM Marco Mipawa amevifahamisha vyombo vya habari nchini kwamba, yeye pamoja na washiriki wenzake 8, wamekubali kwamba kuna umuhimu wa kufanyika mabadiliko makubwa katika sekta ya habari nchni, ili iwe kama ilivyo nchini Ghana.
Mipawa amekiri kufurahishwa na uhuru wa vyombo vya habari nchini Ghana, ambapo huwa vinafanya shughuli zake kwa uhuru mkubwa katika uibuaji wa agenja za kuzuia uovu dhidi ya serikali bila vitisho vyovyote.
Wanahabari wakijiandaa kupanda ndege kutoka Dar es salaam kuelekea Accra via Nairobi |
Naye Meneja wa Jogoo FM Radio ya mjini Songea Magira Magira amesema amejifunza umuhimu wa kutazama kipaji cha mtu katika utangazaji ili jamii imkubali, na kwamba elimu ni kitu cha ziada katika kusaidia kukilinda na kukiboresha kipaji hicho.
Kwa upande wake Meneja Masoko na Mhasibu wa Kahama FM Radio ya mjini Kahama Letcia Kagoro amesema, alichojifunza ni umuhimu wa kuwekeza katika raslimali watu na vitu, kabla ya kuanza uendeshaji wa mradi wowote ikiwemo miradi ya Redio.
Amekiri kwamba, mafanikio yanaweza kufikiwa kwa kuweka malengo ya muda mfupi na mrefu yanayopimika katika uendeshaji wa redio, tv na vyombo vingine; ili kuwa na mwongozo katika utekelezaji wa kazi na tathmini yake.
Wakati huo huo, mkuu wa msafara huo na mmiliki wa Radio CG FM kutoka Tabora Charles George, amewaasa wamiliki na waajiri wa Redio kutambua vipaji vya watumishi wao kabla ya kuwaajiri, kuviendeleza na kuvilinda kwa gharama yoyote.
Naye mwandishi kutoka Triple A FM ya mjini Arusha Marick Munga amesema, alichojifunza ni umuhimu wa vyombo vya habari kufanya tafiti za kina kwa jamii ili kubaini mahitaji yake kabla ya kuibua agenda zinazoihusu.
Meneja wa Standard Radio iliyoko mjini Singida Alice Achieng amefurahishwa na tabia ya ushirikiano wa wafanyakazi katika vipindi mbalimbali redioni na televisheni,ambapo kwa kila kipindi daima huwa pamoja ili kuhakikisha wamepeleka ujumbe ambao jamiia inauhitaji
Timu hiyo ya wanahabari kutoka Tanzania nchini Ghana, jana imemaliza program ya kutembelea kituo cha Multimedia Group LTD kilichoko jijini Accra, ambapo wiki ijayo itatembelea vituo vingine vya habari mjini Kumasi nchini humo.
Wanahabari hao kutoka Tanzania wameahidi kuja kuhamasisha mabadiliko katika uendeshaji wa vipindi vya redio nchini, ili vilenge watu na maisha yao kwa nia ya kufichua uovu na kuwaletea maendeleo.
Ziara ya viongozi tisa wa vyombo vya habari kutoka Tanzania nchini Ghana, ilianza Desemba mosi mwaka huu na wanatarajia kurudi nchini Desemba 15 mwaka huu ambapo mafunzo hayo ya wiki mbili yamefadhiliwa na mfuko wa kusaidia vyombo vya habari nchini TMF.
0 maoni:
Post a Comment