RAIS KIKWETE AHAMISHA WAKUU WA WILAYA 10

RAIS KIKWETE AHAMISHA WAKUU WA WILAYA 10,HUKO MPWAPWA ATEUA MWINGINE!!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemteua Bwana Anthony Peter Mavunde kuwa Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Mkoa wa Dodoma, kuanzia leo, Jumatatu, Mei 25, 2015.

Aidha, Rais Kikwete amefanya uhamisho wa wakuu 10 wa Wilaya kwa nia ya kuongeza ufanisi katika uongozi wa Wilaya mbali mbali nchini.

Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete amemhamisha Luteni Edward Ole Lenga kutoka Wilaya ya Mkalama, Mkoa wa Singida kwenda kuwa mkuu wa wilaya mpya ya Kyerwa, Mkoa wa Kagera. Luteni Lenga anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Luteni Kanali Benedict Kulikela Kitenga ambaye alifariki dunia Aprili 20, mwaka huu, 2015.

Wakuu wengine wa wilaya ambao Rais Kikwete amewahamisha ni Elizabeth Chalamila Mkwasa kutoka Wilaya ya Dodoma kwenda Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro, Dkt. Jasmine Tisike kutoka Wilaya ya Mpwapwa kwenda Wilaya ya Dodoma, Agnes Elias Hokororo kutoka Wilaya ya Namtumbo, Mkoa wa Ruvuma kwenda Wilaya ya Tunduru, mkoani humo humo na Fadhili Nkurlu kutoka Wilaya ya Misenyi, Mkoa wa Kagera kwenda Wilaya ya Mkalama.

Wengine ambao wamehamishwa ni Chande Bakari Nalicho kutoka Wilaya ya Tunduru kwenda Wilaya ya Namtumbo, Festo Shem Kiswaga kutoka Wilaya ya Mvomero kwenda Misenyi, Darry Ibrahim Rwegasira kutoka Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera kwenda Wilaya ya Biharamulo, mkoani humo humo, Elias Choro John Tarimo kutoka Wilaya ya Biharamulo kwenda Chunya, Mkoa wa Mbeya na Deodatus Lukas Kinawiro kutoka Wilaya ya Chunya kwenda Wilaya ya Karagwe, Mkoa wa Kagera.
 
Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
25 Mei, 2015

0 maoni:

Post a Comment