Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanadaiwa kumzuia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad kuhudhuria shughuli ya kuvunjwa kwa Baraza hilo inayotarajiwa kuongozwa na Rais wa Zanzibar Dk.Ali Mohamed Shein kesho, kufuatia kitendo cha Mawaziri na Wawakilishi wa CUF kususia kupitisha bajeti kuu ya Serikali ya mwaka wa fedha 2015/16.
Azimio hilo limetolewa na wajumbe wa Chama cha Mapinduzi, baada ya Spika wa baraza la wawakilishi Pandu Ameir Kificho kuwataka wajumbe wa baraza hilo kutengua kanuni ili kuruhusu viongozi wa kitaifa akiwemo Rais wa Zanzibar, Makamu wa Kwanza wa Rais na Jaji Mkuu waruhusiwe kuingia ndani ya ukumbi wa baraza wakiwa kama wageni waalikwa.
Wakizungumza mara baada ya azimio hilo kupitishwa, Kaimu Mnadhimu wa Baraza hilo wa CCM, Ali Salum Haji, Mwakilishi wa viti maalum Asha Bakari na Mwakilishi wa jimbo la Raha Leo Nassor Salum Aljazeera wamesema hakuna sababu ya kumruhusu Maalim Seif kuhudhuria shughuli hiyo wakati Mawaziri na Wawakilishi wanaotokana na chama chake cha CUF wakiwa wamegoma kuhudhuria shughuli za baraza hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mambo ya Nje na Mwakilishi wa jimbo la Mji Mkongwe wa CUF, Ismail Jussa Ladhu amesema tayari chama chake kimeanza kuchukua hatua kwa kuziandikia barua taasisi zenye dhamana na mambo ya uchaguzi, vyombo vya dola na jumuiya za kimataifa kuhusu ukiukwaji wa taratibu za uchaguzi unavyofanyika Zanzibar na dhamira ya wajumbe wa CCM ya kutaka kuvunja Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
0 maoni:
Post a Comment