WAALIMU WABAKWA,WADHALILISHWA,HUKO BUNDA!!!!!

MBUNGE wa Mwibara, mkoani Mara, Bw. Kangi Lugola, amelazimika kukatisha vikao vya Bunge vinavyoendelea Mjini Dodoma na kwenda jimboni kwake, Kijiji cha Nambaza, Kata na Tarafa ya Nansimo, wilayani Bunda, ili kushughulikia adha wanayoipata walimu
wa shule ya msingi kijijini hapo.

Walimu hao wanadaiwa kufanyiwa vitendo vya kishirikina kwa kuteswa, kudhalilishwa hivyo kulazimika kuomba uhamisho ili wakafundishe shule nyingine zilizopo mbali na jimbo hilo.

Wakisimulia vitendo wanavyofanyiwa, walimu hao walisema usiku wakiwa wamelala, wachawi huwafuata na kuwanyoa nywele sehemu za siri, kuwaingilia kimwili, kuwaibia mali pamoja na fedha zao.

Walisema mbali ya vitendo hivyo, pia wamekuwa wakikuta mikojo, ugali na samaki ukiwa umefunikwa na shuka kitandani hali ambayo imewafanya washindwe kufundisha na kuomba wahamishwe.

Mwalimu Joyce Maugo ambaye ni mkongwe katika shule hiyo, alisema walimu wa shule hiyo wako hatarini kutokana na vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa ambapo mmoja wa walimu wa kike ambaye kimaumbile ni mdogo, aliingiliwa kishirikina hadi akazimia.

Alisema asubuhi alipoitwa kwenda kushuhudia yaliyomkuta mwalimu huyo, alikuta amefanyiwa mambo ya aibu akiwa hawezi kutembea ambapo kitandani kulikuwa na damu, mikojo na kinyesi.

Aliongeza kuwa, mwalimu mwingine wa kiume, Pasco Mayamba, alikuwa amefunga milango na madirisha ya chumba chake lakini asubuhi alipoamka, alikuta madirisha na milango iko wazi, kitanda kimejaa mikojo, ugali, kipande cha mnofu wa sangara na mchuzi.

"Wakati mwingine tukila chakula usiku kinabadilika, kama ulikuwa wali na nyama unakuwa ugali na dagaa au mboga za majani hali ambayo ni ya mateso makubwa, kama kuna makosa tumefanya bora tuambiwe ili tuombe msamaha badala ya kuendelea kututesa na kutunyima amani ya kazi na maisha," alisema Bi. Maugo.

Mwalimu mwingine aliyefahamika kwa jina moja la  Lucy, alisema mbali ya kupata adha hiyo, wachawi hao huwaibia fedha, vitambulisho, kadi za benki na mali nyingine na wakati mwingine hukuta mikojo na kinyesi kwenye madebe ya unga na chungu cha mboga vitendo ambavyo vinawanyima morali ya kazi.

"Kuna wakati tunakuta vinyesi madarasani jambo ambalo huwalazimu wanafunzi na walimu kuvizoa na kufanya usafi...tunawaomba viongozi wa kijiji wachukue hatua dhidi ya vitendo hivi," alisema.

Akizungumza na gazeti hili Mjini Bunda, Bw. Lugola alisema vitendo vya kishirikina wanavyofanyiwa walimu hao si vya kufumbiwa macho bali vinapaswa kukemewa na wahusika wakibainika wachukuliwe hatua kali kwani mbali na madhara wanayoyapata walimu ikiwa ni pamoja na kuingiliwa kimwili, vitendo hivyo vinawadhalilisha na kudidimiza maendeleo ya elimu jimboni humo.

"Nimelazimika kwenda Kijijini Nambaza kushughulikia tatizo hili na kesho (leo), nitafanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kijiji hicho ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo liweze kukoma lisitokee tena," alisema.

Hivi karibuni, wakazi wa kijiji hicho walifanya mkutano wa hadhara na kuwapigia kura baadhi ya wanakijiji ambao wanadaiwa kuwa wahusika wakuu wa kufanyia walimu hao vitendo vya kishirikina na kinara wa mambo hayo inadaiwa ni kiongozi wa kijiji hicho ambaye anaishi jirani na shule hiyo.

Katika mkutano huo, wanakijiji waliazimia wahusika hao wahame haraka kijijini hapo kabla hawajachukua sheria mkononi wakidai
vitendo wanavyovifanya mbali na kuvunja sheria vitasababisha shule yao ikose walimu wa kuwafundisha watoto wao hali ambayo  inaweza kusababisha kijiji kukosa wasomi.

Akizungumzia uamuzi wa kijiji hicho, Bw. Lugola alisema anayaheshimu maamuzi hayo na kabla wananchi hawajafikia hatua ya kuchukua sheria mkononi atawashauri watu hao wahame kijiji hicho haraka.

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Milumbe, aliliambia gazeti hili kuwa vitendo hivyo hawezi kuvivumilia kwani ni udhalilishaji ambao Wilaya haiwezi kuufumbia macho hivyo lazima achukue hatua.

Alisema atakwenda Nambaza kuzungumza na wananchi wa kijiji hicho ambapo kwa mamlaka aliyonayo kwa mujibu wa sheria, atachukua hatua kali dhidi ya wote ambao watabainika kuhusika na vitendo hivyo vya kihuni na kusisitiza atayaheshimu maamuzi ya wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Bi. Lucy Msofe, alisema, amesikitishwa na vitendo wanavyofanyiwa walimu hao ambao umri wao ni mdogo ambapo huo ni ukatili wa hali ya juu.

"Tayari nimelazimika kumuhamisha mwalimu mmoja wa kike ambaye alifika kwangu akiwa na hali mbaya kutokana na vitendo alivyofanyiwa na watu hao...kama hali hiyo itaendelea, nitawahamisha walimu katika shule hiyo na kuwapeleka shule zenye mahitaji kwa sababu huenda shule hii ya Nambaza haiwataki," alisema.

Aliongeza kuwa, hayuko tayari kuendelea kushuhudia watoto wa watu wakiendelea kuteseka, kunyanyasika, kudhalilishwa na kufanyiwa unyama kiasi hicho akidai atawahamisha kama vitendo hivyo havitakomeshwa.

0 maoni:

Post a Comment