JESHI la Polisi mkoani Tabora, limewakamata na kuwafikisha mahakamani watu sita, kwa tuhuma za kukutwa na mifupa sita ya binadamu, inayodhaniwa kuwa ni ya watu wenye ulemavu wa ngozi (albino).
Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Suzan Kaganda alisema watuhumiwa hao walikamatwa asubuhi ya Mei 22, mwaka huu wilayani Igunga.
Kaganda aliwataja watuhumiwa hao wanaodaiwa kukiri kujihusisha na matukio ya kudhuru albino kuchukua viungo kuwa ni Mussa Njile (30), mkazi wa Mnale, Elizabet Masanja (42), mkazi wa Bungwa.
Wengine ni Bahati Kilungu (56), ambaye ni mwalimu na mkazi wa Mbutu Kahama, Bilia Masanja (38), mkazi wa Bukene wilayani Nzega, Muhoja John (28), mkazi wa Nyasa na Rejina Kashidye (40), mkazi wa Isegenhe.
Kamanda Kaganda alikumbushia tukio la Agosti 16, mwaka jana, katika kitongoji cha Mikese kijiji cha Buhelela wilayani Igunga mkoani hapa la kuuawa kwa Mapambo Mashiri aliyekuwa amelala nyumbani kwake na mkewe, Mungu Masanja, mwenye ulemavu wa ngozi, aliyekatwa mkono wa kushoto na watu wasiojulikana, kisha kutokomea nao.
Alisema, kuwa watuhumiwa hao walipohojiwa na Polisi walikiri kuhusika katika tukio hilo pia.
“Kufuatia kuendelea kwa matukio hayo, Jeshi la Polisi mkoani hapa linaendelea kuwasaka wanaojihusisha na vitendo vya kudhuru albino. Msako utaendelea tuwatie nguvuni na kuwachukulia hatua za kisheria".
Katika hatua nyingine, Kamanda huyo alisema kuwa, watu hao walifikishwa mahakamani Juni 3, mwaka huu kwa kuhusika na matukio mawili, likiwemo la kujaribu kuua kwa kumkata mkono, mtoto Nkamba Ezekiel kwenye kijiji cha Mwisole, Kata ya Lutende, Julai mwaka jana.
0 maoni:
Post a Comment