Na YOHANA EMMANUEL
MARA kadhaa tulishuhudia namna wasanii wa bongo fleva na bongo movie walivyokuwa karibu na utawala wa rais mpendwa anayemaliza muda wake Dk. Jakaya Mrisho Kikwete.
Dhifa mbali mbali zilizofanyika Ikulu zilijaza wasanii hao wa bongo fleva na bongo movie huku wale wa dansi na taarab wakiwa ni wa kutafuta kwa tochi.
Sijui kama ni kwa ubora wa kazi zao au namna wanavyojua kujipanga na kujipenyeza kwenye maeneo muhimu au ni mapenzi binafsi ya mkuu wa nchi, lakini ukweli ni kwamba iwe ni sababu yoyote ile, awamu ya nne ilikuwa rafiki ya wasanii wa filamu na muziki wa kizazi kipya.
Historia inaonyesha wazi kuwa Rais Kikwete alikuwa mshabiki wa muziki wa muziki wa dansi, Sikinde ikihusishwa zaidi, lakini mwisho wa siku karata ikabadilika.
Ukaribu wa Ikulu na wasanii hao wa bongo fleva na filamu kumesaidia sana kupandisha hadhi yao na kuongeza heshima ya kazi zao, kilio chao kimekuwa kikisikika kirahisi huku makongamano yao mara kadhaa yakipewa sura ya kitaifa.
Ukiondoa msiba wa Muhidin Maalim Gurumo uliopata sura ya kitaifa na kuhudhuriwa na viongozi wengi wa serikali, misiba mingi ya wasanii wa taarab na dansi imekuwa ni ile isiyopata bahati ya kuhudhuriwa hata na Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa.
Unakumbuka msiba wa Kanumba ulivyokuwa? Sharo Milionea, Mangwea, George Tyson, Adam Kuambina na Mzee Small na wengineo? – Ilikuwa na sura ya misiba ya kitaifa.
Unakumbuka kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 namna zilivyojaa wasanii wa bongo fleva waliokuwa wakilipwa pesa nene? –dansi na taarab zilipigwa chini pengine ni kwasababu ile ile ya kutokuwa na ukaribu na Ikulu.
Wanamuziki wa dansi na taarab ndio wanaoishi katika mazingira magumu kwa kutegemea kiingilio cha mlangoni kupitia maonyesho yao ya kila wiki ambayo mahudhurio yake si ya kujivunia.
Kazi ngumu siku tatu hadi tano kwa wiki, kwenye kumbi zisizoisha misukosuko ya vibali huku kipato kikiwa kiduchu, ndiyo maisha ya karibu bendi zote za dansi na taarab, japokuwa dansi ina balaa pia la kutengwa na vyombo vingi vya habari.
Hakika dansi na taarab ni miziki inayohitaji mbeleko ya serikali vinginevyo itapotea kabisa kwenye soko la muziki na itabaki kuwa historia.
Najaribu kufikiria iwapo rais ajaye atakuwa na uswahiba wa muziki wa dansi na taarab na kwa bahati mbaya hadi sasa rais mtarajiwa ni mmoja tu – Dr John Pombe Magufuli kupitia CCM. Vyama vingine bado havijataja wagombea wao.
Nikimtazama Magufuli nafarijika na kujipa imani kuwa hana sura ya bongo fleva wala bongo movie – namuona ana sura ya muziki wa dansi.
Mara mbili katika matukio mawili nimebahatika kumshuhudia kupitia televisheni akizicharaza tumba (ngoma) za muziki wa dansi katika matukio ya kiserikali.
Lakini siyo kupiga tu, bali ulikuwa unaona kabisa namna anavyozijua tumba, namna anavyosikia raha kuzipiga na namna anavyojivunia kushiriki kwenye burudani hiyo – Pengine marais wote watarajiwa wakiwa kama Magufuli basi angalau neema inaweza kupatikana kwenye muziki wa dansi na taarab. Tuombe Mungu iwe hivyo.
0 maoni:
Post a Comment