RAIS Jakaya Kikwete, amewataka viongozi wa dini nchini kutowapa mwanya wanasiasa wenye dhamira ovu ya kuwafarakanisha Watanzania bali waendelee kukemea matumizi mabaya ya fedha, rushwa na hujuma katika Uchaguzi Mkuu hasa kipindi hiki.
Alisema ipo haja ya viongozi hao kuendelea kuwakemea wanasiasa wanaopenda madaraka kwa gharama yoyote wakitumia fedha kununua ushindi au ubaguzi wa rangi, kabila, dini, kuwabagua wapinzani wao na kujijenga zaidi kisiasa.
Rais Kikwete aliyasema hayo jana katika Maadhimisho ya Miaka 125 ya Injili katika Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), yaliyofanyika katika Viwanja vya Mbuyukenda, mkoani Tanga.
Aliwaomba viongozi wa dini na wananchi, wasiwasikilize wanasiasa wenye dhamira ovu wala kuwaendekeza kwani mchezo wao ni mauti ya Watanzania hivyo wawakatalie kwa macho makavu.
Alisema si vyema kukaa kimya dhidi ya watu wanaokiuka maadili na kuchochea mifarakano katika Taifa kwani watu hao si wema bali wataifikisha nchi pabaya hivyo wasiruhusiwe kuchezea dini zetu ambazo ni mhimili muhimu wa amani yetu tofauti na ukabila.
"Tusikubali kumchukiza Mungu akatukasirikia na kutuadhibu kwa jambo ambalo liko ndani ya uwezo wetu kulizuia lisitokee, mambo yakiharibika hatuwezi kumlaumu mtu mwingine yeyote bali sisi wenyewe.
"Katu hatuwezi kusema ni mapenzi ya Mungu bali itakuwa ni makosa yetu wenyewe, nawaomba viongozi wa dini mlisaidie Taifa letu, limeni mraba wenu vizuri nasi tulime wetu, msiwape nafasi viongozi wa siasa na hata wa dini kutumia majukwaa ya dini kuendeleza maslahi yao
ya kisiasa hasa kupandikiza chuki katika jamii," alisema.
Rais Kikwete aliongeza kuwa, Serikali inawategemea viongozi wa dini wasiwe sehemu ya makundi ya wagombea au vyama vya siasa bali wanapaswa kuwa pande zote ili waweze kufanya vizuri kazi yao ya kuliponya Taifa kama kutatokea matatizo.
Aliongeza kuwa, Serikali haitegemei viongozi wa dini wawapangie waumini wao vyama au viongozi wa kuwachagua bali wawahimize na kuwakumbusha waweze kutumia haki na wajibu wao vizuri.
"Muwakumbushe mambo muhimu matatu, kwanza kujiandikisha, pili, kujitokeza kwenda kupiga kura, tatu kuchagua viongozi wazuri wasio waovu, wasiofanana na uovu na kuukaribia uovu, watakaosukuma mbele gurudumu la maendeleo na kujali maslahi mapana ya jamii husika na nchi yetu," alisema Rais Kikwete.
Aliwaomba waendelee kuiombea Tanzania iendelee kuwa ya amani na utulivu ili watu wake wadumishe upendo na mshikamano miongoni mwao na kuombea Uchaguzi Mkuu ujao uwe salama ili Taifa lipate viongozi wazuri, liendelee kuwa tulivu kabla, baada ya uchaguzi.
Alisema historia inaonesha kuwa, katika nchi nyingi za Afrika wanasiasa hutumia kupindi cha uchaguzi kufanya maasi hivyo uadilifu na tahadhari kubwa inahitajika.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa hilo Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Dkt. Stephen Munga, alisema ili Taifa liweze kuvuka kipindi cha uchaguzi salama, Uchaguzi Mkuu ufuate misingi yote iliyowekwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ili kuwapa uhuru wananchi waweze kuchagua viongozi wanaowataka.
0 maoni:
Post a Comment