"CCM ITASHINDA KWA KISHINDO KIKUBWA HILO NAWAAHIDI"-Magufuli



Waziri wa Ujenzi na mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amesema kuwa wana-CCM mwaka huu wanapaswa kufanya kampeni za kisayansi zaidi kuhakikisha wanapata ushindi wa tsunami utakaowezesha kuundwa kwa Serikali imara itakayowaletea maendeleo Watanzania wote.

Alisema kwa kufanya hivyo kutawasaidia kupata viti vingi na kusimamia shughuli zote za maendeleo na kwa manufaa ya wanaCCM na Watanzania wote kwani mahitaji yao na matarajio yao ni kupata maendeleo makubwa.

“Niwaombe wana CCM wenzangu, tushikamane tuwe wamoja. Kampeni za mwaka huu ni lazima tufanye kampeni za kisayansi zaidi, ni lazima kampeni zianze katika ngazi ya nyumba kumi, vitongoji kwa vitongoji, vijiji, mitaa, kata majimbo , wilaya, mikoa na baadaye urais kwa ujumla. Katika umoja huu nataka niwahakikishie ushindi wa mwaka huu wala si wa kimbunga, ni wa tsunami,” alisema Dk Magufuli.

Dk Magufuli aliyekuwa katika ziara ya mikoa ya kusini ya kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyotelekezwa katika kipindi cha awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, alisema hayo hapo jana wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho nje ya ofisi za CCM mkoa wa Mtwara, ikiwa ni siku moja baada ya rais kukamilisha ziara yake na kuwaaga wananchi wa mkoa huo.

Mgombea huyo na mbunge wa Chato alibainisha kuwa amekuwa kiongozi katika maeneo mbalimbali nchini kwa kipindi kirefu, hivyo anakifahamu vema chama, shida za wanaCCM na matarajio yao yanayojumuisha matarajio ya Watanzania wote na shida zao.

Alisema kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais, hatawasahau wanaCCM na Wanamtwara kwa ujumla, lakini wote hao wanapaswa kushikamana na kuwa kitu kimoja kwa kuwa maendeleo hayana chama na akichaguliwa atakuwa rais wa Watanzania wote.

Alisema katika kipindi cha miaka 20 ya uongozi, amekuwa akifika Mtwara na hivyo ana uhakika endapo Wanamtwara wataamua kumpatia nafasi ataujua zaidi mkoa huo kuuendeleza katika kipindi cha miaka mingine zaidi.

“Wanamtwara nafahamu matarajio yenu, nataka niahidi kwenu na nimwombe Mungu nitapenda sana niwe mtumishi wa watu, nisiwe na majivuno wala kujiona, niwe mtumishi hasa wa wanyonge niweze kuwasikiliza na kusikiliza matarajio yao.

“Matarajio ya Watanzania na Wanamtwara ni makubwa, wanahitaji maendeleo makubwa na tunahitaji kuyasukuma. Nchi yetu imelelewa katika misingi ya umoja pasipo kubaguana kutokana na maeneo tunayotoka, dini, makabila hivyo tunahitaji umoja na palipo na umoja pana amani na palipo na amani pana maendeleo,” alisema Dk Magufuli.


Makundi ndani ya vyama


Akizungumzia makundi katika chama hicho, alisema yalikuwapo zaidi ya 40 na baada ya uchaguzi makundi yote yalimuunga mkono yeye aliyepitishwa na vikao vya chama, hivyo wanaoondoka ndani ya chama hicho kwa chama kikubwa kama CCM ni jambo la kawaida kwa kuwa hata enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere wapo walioondoka na waliofukuzwa.

“Mti ambao unataka upate mbao zake nzuri, matawi kudondoka ni neema, lakini kwa watu kuondoka ndani ya CCM ni kawaida na kwa chama kikubwa kama CCM ni jambo la kawaida sana,” alisema Dk Magufuli.


Mtwara wajipanga


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mtwara, Homamed Sinani alisema watahakikisha CCM Mtwara inaendelea kupata ushindi wa kishindo kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais.

“Chama kipo imara, mimi kama mwenyekiti wa chama mkoa nasema chama kimejipanga kikamilifu na nina imani kama mshikamano ukidumishwa tunatarajia ushindi wa vishindo kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge hadi urais,” alisema Sinani.

JK akemea siasa chafu


Katika hatua nyingine, wakati akihitimisha ziara yake juzi, Rais Kikwete aliwataka wanasiasa mkoani Mtwara kuacha siasa chafu za kupotosha wananchi badala yake wawaambie ukweli juu ya miradi na mikakati ya maendeleo inayoendelea mkoani humo.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo juzi wakati akiweka jiwe la msingi katika tawi la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tawi la Mtwara ambalo ni la saba nchini na baadaye kuirudia wakati akihutubia mkutano wa kuwaaga wananchi.

Rais Kikwete aliwataka wananchi kutosikiliza maneno ya watu wapotoshaji wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kwa bei nafuu.

Alisema kuwa hakuna mtu yeyote anayeweza kuzuia maendeleo ya Mtwara kwa sababu kuna fursa nyingi zinazovutia uwekezaji.

“Msisikilize maneno ya wapotoshaji wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kwa bei nafuu, Mtwara na Lindi kulichelewa lakini kutakuwa kwa kwanza na kule kulipokuwa kumetangulia kutafuata,” alisema Rais Kikwete.
Ingawa hakufafanua, kauli hiyo ya Rais Kikwete ilikuwa inalenga vurugu za wananchi wa Mkoa wa Mtwara zilizotokea mwaka jana zikipinga usafirishaji wa gesi kwa njia ya bomba kwenda Dar es Salaam ambazo zilihusishwa na ushawishi wa kisiasa.

Hata hivyo alisema kuwa Mtwara ndio muhimili mpya wa uchumi wa Tanzania kutokana na kuwa na rasilimali nyingi zinazotoa fursa za uwekezaji hivyo kunahitajika uwepo wa huduma za kibenki kwa karibu.

“Wanasiasa wa Mtwara msiwachanganye wananchi badala ya kuwaeleza msimamo sahihi wenye mwelekeo mnakwenda kuwapeleka kwenye mambo ambayo yanawaongezea sifa ya muda mfupi na kuwavuruga wananchi hawa na kukosa utulivu wa kufanya mambo ya maana,”alisema Rais Kikwete.


Gavana: Tumepiga hatua


Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu alisema Tanzania imepiga hatua katika matumizi ya teknolojia ya huduma za simu za mkononi za kibenki zenye gharama nafuu na kuingia katika nafasi ya kumi duniani na namba moja kwa Afrika.

Profesa Ndulu alisema BoT wamekuwa wakitumia vituo maalumu vya kusambazia fedha na inapobainika kuongezeka kwa mahitaji ya sarafu kwa kuzingatia ongezeko la shughuli za kiuchumi katika eneo fulani hufungua tawi kama ilivyofanyika Mtwara.

Alisema kulingana na tathimini mbalimbali za matumizi ya huduma za kifedha nchini, hadi kufikia mwaka 2006 asilimia tisa ya Watanzania walifikiwa na huduma rasmi za kifedha za benki na zile zisizokuwa za kibenki.

Alisema hadi Machi 2015, idadi ya akaunti za huduma za kifedha kupitia simu za mikononi ilifikia 40.7 milioni huku Watanzania milioni 26.8 sawa na asilimia 95 wakiwa na akaunti za matumizi ya fedha kwenye simu zao.

0 maoni:

Post a Comment