MWANAMKE ATALIWA NA FISI ,WAWILI WAJERUHIWA!!!!!


Hofu imetanda kwa wakazi wa halmashauri ya Mji wa Bariadi Mkoani Simiyu, baada ya kukithiri kwa  matukio ya watu kushambuliwa hadi kufa na wanyama aina ya fisi katika maeneo ya mbalimbali mjini Bariadi.

Hofu hiyo imetanda zaidi hasa baada ya mwanamke mmoja ambaye hakufahamika mara moja jina, umri wala  mahali anapoishi kuvamiwa kisha kuliwa na fisi , Agosti 16,2015 majira ya jioni, katika Mtaa wa Kidinda  Mjini Bariadi.

Walioshuhudia tukio hilo wamesema mwanamke huyo alikuwa akivuka mto katika mtaa huo na kwamba huenda wakati anavuka ndipo alivamiwa na fisi huyo kusababisha kifo chake.

Hata hivyo  kifo cha mwanamke huyo kimezua utata kutokana na baadhi ya watu kudai kuwa siyo kawaida fisi kumsababishia kifo mtu mzima kwa sababu mara nyingi fisi wana tabia ya kukamata watoto wadogo huku wakidai kuwa inatokana na imani za kishirikina.

Wakiongea na Malunde1 blog mashuhuda wamesema hivi sasa hali ni mbaya katika mji wa Bariadi kutokana na matukio hayo ya watu kuliwa na fisi kuongezeka, ambapo ndani ya mwezi mmoja watu wanne wameliwa na fisi  katika eneo hilo.


“Ndani ya mwezi huu watoto watatu wameliwa na fisi hapa hapa mjini, leo huyu mama naye kaliwa na fisi…tunajiuliza kuna nini hapa? Je ni kweli hawa ni fisi wa kawaida?  Hatujawahi kuona fisi anamvamia mtu mzima na kumsababishia kifo”, ameeleza Ezron James.

" Hili ni tukio la kwanza na la aina yake..hakuna fisi  anayeweza kumkamata mtu mzima... fisi wengi hukamata watoto wadogo ,fisi anaogopa watu wazima ...inakuwa je kwa huyu mam, tena mtu mzima? ninavyofikiri pengine mwanamke huyu aliuawa na mtu kisha akatupwa maeneo haya na fisi wakati wa pita pita zao wakamkamata na kumtafuna" ,ameongeza shuhuda mwingine.

Katika hatua nyingine wananchi hao wameituhumu idara ya wanyama pori katika halmashauri hiyo kwa kushindwa kutatua hali hiyo, kutokana na kukaa kimya huku watu wakiendelea kupoteza maisha.

Aidha wameitaka serikali kufanya uchunguzi wa kina juu ya kuwepo kwa matukio hayo, kutokana na watu kuendelea kupoteza maisha kwa kuvamiwa na wanyama hao.

“ Tunaishangaa ofisi ya maliasili wilaya hakuna jambo walilofanya wakati watu wanaendelea kupoteza maisha….tunaomba waingilie kati…angalia jamani ndugu zetu wanapoteza maisha kwa sababu ya fisi... fisi... fisi kila siku…mbona zamani walikuwepo lakini hali hii haikuwepo?...hawa siyo fisi wanyama ni fisi watu” ,wamesema wakazi wa eneo hilo.

Wameongeza kuwa kutoka na matukio hayo ya fisi, hivi sasa baadhi ya wananchi katika mji huo wanaogopa kutembea nyakati za jioni na usiku, muda ambao fisi hao wanavamia watu na kuwasababishia kifo huku wakiwanyofoa nyama katika sehemu mbalimbali za mwili yao.

Akiongelea hali hiyo pamoja na ofisi yake kulalamikiwa kwa kutochukua hatua, Afisa maliasili katika halmashauri hiyo Hellena Lintu amesema ofisi yake imeshindwa kutatua hali hiyo kutokana na kutokuwa na uwezo wa kupambana na wanyama hao.

“ Jamani waandishi wa habari sisi hatuna njia ya kufanya…hata sisi hapa ofisini tumeshindwa tufanye nini…tukiamua kufanya msako hakuna fisi ambaye unaweza kumkamata…hatujui hao fisi wanajificha wapi  ” ,amesema Lintu.

Naye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ambaye pia ni Mkuu wa wilaya ya Bariadi Ponsiano Nyami amesema amepata taarifa za kuwepo kwa hali hiyo huku akibainisha kuwa tayari ameitisha kikao cha kamati ya ulinzi na usalama ili kuweza kuweka mikakati ya kupambana na wanyama hao.

“ Kabla ya kamati ya ulinzi na usalama nimekaa kikao na maofisa wanyamapori katika halmashauri hiyo…tumeweka mikakati mbalimbali na tutaanza msako mkali wa kupambana na fisi hao” ,amesema Nyami.

Jitihada za waandishi wa habari kumtafuta Kamanda wa polisi Mkoa wa Simiyu Gemin Mushy ofisini kwake ili kuthibitisha kutokea kwa kifo cha mwanamke huyo, ziligonga mwamba kwa madai kuwa Kamanda huyo yupo katika shughuli za ukaguzi.

Hata hivyo alipotafutwa kwa njia ya simu kuzungumzia tukio hilo, kamanda Mushy amesema kuwa hana taarifa za kuwepo kwa tukio hilo licha ya askari polisi kituo cha Bariadi Mjini kufika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu na kuupeleka katika hospitali ya wilaya.

0 maoni:

Post a Comment