Safari Ya Rais Uhuru Kenyatta Wa Kenya Nchini Uganda

Safari ya Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya nchini Uganda
Jumamosi, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliwasili mjini Kampala, mji mkuu wa Uganda kwa safari rasmi ya kikazi.

 Lengo la safari hiyo, ni kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa Uganda kuhusiana na masuala muhimu ya kieneo ukiwamo mgogoro wa kisiasa nchini Burundi, machafuko yanayoendelea nchini Sudan Kusini na pia hali ya usalama nchini Somalia. 

Leo Jumatatu sawa na tarehe 10 Agosti, Rais Kenyatta atakuwa na kikao na Marais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan, Yoweri Museven wa Uganda na Hailemariam Desalegn Waziri Mkuu wa Ethiopia. Kikao hicho kitafanyika Entebbe. Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imetangaza kwamba, viongozi wa nchi hizo nne watajadili njia za utatuzi wa migogoro ya eneo hilo.

Kenya na Uganda ni miongoni mwa nchi waasisi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambayo ilihuishwa tarehe saba mwezi Julai mwaka 2000. Uganda na Kenya pia ni miongoni mwa nchi za eneo la Maziwa Makuu ya Afrika. Nchi hizo zinaunganishwa na mambo mengi ya kiutamaduni, lugha na kadhalika ambavyo vyote vinachangia katika kuimarisha mashirikiano ya kisiasa na kiuchumi ya pande hizo mbili.

Hata hivyo weledi wa mambo wanaamini kwamba, licha ya kuwepo ushirikiano na  uhusiano huo, viongozi wa nchi hizo mbili wanashindana kwa ajili ya kuwa na nafasi muhimu na ushawishi mkubwa zaidi katika eneo la mashariki mwa Afrika.
Kugunduliwa akiba ya mafuta katika nchi za Kenya na Uganda mwaka uliopita, kuliibua maswali katika uga wa kisiasa barani Afrika kwamba, je nchi hizo mbili baadaye zitakuwa miongoni mwa nchi wauzaji nje wa mafuta?

Wakati huo huo ni wazi kuwa Kenya na Uganda zinahitajia kuwa na amani na utulivu mkubwa kwa ajili ya kuchimba mafuta na kuuza bidhaa hiyo katika nchi nyingine na pia kwa ajili ya kushirikiana na masoko ya kimataifa. Hasa kwa kuzingatia kuwa, viongozi wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki wametiliana saini makubaliano ya kuanzisha eneo huru la kibiashara na viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Soko la Pamoja la Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA). Hivyo basi ili lengo hilo litimie nchi hizo zinatakiwa kwanza kuhitimisha machafuko na rangaito kati ya nchi wanachama wa taasisi hizo.

Itakumbukwa kuwa mashambulizi ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al Shabab nchini Somalia yamekuwa na taathira hasi kwa usalama wa nchi za eneo la Pembe ya Afrika kama vile Ethiopia. Vilevile kuendelea machafuko ya kisiasa katika nchi za Burundi na Sudan Kusini ni jambo jingine lililoathiri usalama wa ndani wa nchi za Afrika Mashariki kama Kenya na Uganda.

Ni kwa kuzingatia hali hiyo ndiyo maana viongozi wa nchi za Kenya na Uganda, wakapanga kukutana na Rais Omar Hassan al-Bashir wa Sudan na Waziri Mkuu wa Ethiopia,  Hailemariam Desalegn kwa lengo la kujadili njia za utatuzi wa migogoro ya nchi za eneo hilo.

0 maoni:

Post a Comment