"SIKUJUA KUWA NYUMA YANGU NINAO WAUNGWANA WENGI KIASI HIKI,ASANTENI...!!"- LOWASSA


Mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa, anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Watanzania, amekiri kuona maajabu Muleba kwa idadi kubwa ya wananchi waliojitokeza kumpokea na kumsikiliza.

Akizungumza na umati wa wakazi wa Muleba katika uwanja wa Fatuma uliopo jirani na stendi ya mabasi jana, Lowassa alisema anachokiona ni maajabu. 

“Naona maajabu, naona maajabu makubwa. Sikuamini nyuma yangu nina waungwana kiasi hiki...sikujua Muleba mna mahaba kiasi hiki.
“Itoshe tu kusema nimefurahi sana na asanteni sana,” alisema.

“Tumepita maeneo mbalimbali nchini hali niliyoikuta ni kama hii hapa ya Muleba, Mungu anipe nini miye. Asanteni sana.

“Umma huu niliouona nina haja kweli ya kuomba kura, basi naomba kuwashukuru, lakini hata hivyo nawaombeni kura zenu,” alisema. Alisisitiza kuwa anao uwezo wa kuongoza nchi kwa spidi ya kasi na anataka kupambana na umaskini mkubwa uliokithiri tangu 1962.

Mapema Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, alisema hakuna sababu kwa Watanzania kuing’ang’ania CCM ibaki madarakani ili waje kufa nayo bali wametaka wamwachie Dk John Magufuli kufa nayo.

“CCM lazima idondoke mwaka huu, imewapumbaza Watanzania kwa muda mrefu kiasi cha wananchi kudhani kwamba upande wa pili nje ya CCM hakuna maisha na wametuwekea pazia jeusi ili tusione. “Sasa sisi tumetoka CCM na kuja huku ili kulitoboa hilo pazia jeusi,” alisema. Alisema wao walikuwa CCM na wana uzoefu wa utawala lakini wametoka hivyo hakuta kuwa na matatizo kama ambavyo CCM inavyowatisha wananchi kuwa wakichagua upinzani kutakuwa na machafuko.

“CCM ni waongo na wanang’ang’ania madaraka...kitakachoingiza nchi katika matatizo sio kukichagua chama cha upinzani bali chama tawala kung’ang’ania madaraka.

Alisema kila chama kina nadi sera zake kwa wananchi kuhusu masuala ambayo kitawatekelezea kwa kipindi cha miaka mitano ijayo, sasa kama chama hicho kimeshindwa kufanya hivyo, wananchi wana haki ya kukiondoa madarakani kwa kukinyima kura.

0 maoni:

Post a Comment