Mashirika ya dini ni miongoni mwa taasisi zilizotakiwa kuwasilisha nyaraka kwa ajili ya kuhakiki kama yalilipa ushuru wa bandari uliosababisha Serikali kupoteza Sh48 bilioni.
Uwapo wa taasisi hizo za kiimani kwenye sakata hilo ulibainishwa jana katika orodha ya iliyotangazwa jana na Mamlaka ya Bandari (TPA) ambayo ina kampuni na taasisi 40 zaidi ya orodha iliyotangazwa juzi yenye kampuni 243. Kwa tangazo la jana, kampuni na taasisi zinazotakiwa kuwasilisha nyaraka kuhusu malipo hayo sasa ni 283.
Tangazo la TPA lilitolewa jana likiwa na tarehe ya Desemba 24, linazitaka taasisi hizo ambazo ni Baraza la Kikristo Tanzania (CCT) na Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki, Caritas Tanzania na nyingine 281 kwenda kuchukua barua zao kwa ajili ya uhakiki wa malipo ya ushuru huo yaliyofanyika kuanzia Julai 2014 hadi Aprili, 2015.
Taasisi nyingine maarufu zilizopo katika orodha hiyo ni klabu maarufu ya mchezo wa soka ya Azam Football, kampuni maarufu ya Toyota Tanzania Ltd na Bakhresa Food Products.
Juzi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa alizihusisha baadhi ya taasisi hizo 283 na upitishaji wa makontena 11,884 na magari 2,019 kwenye bandari bila kulipia ushuru wa bandari.
Kubainika kwa ukwepaji huo ushuru, kunafanya idadi ya makontena yaliyohusika katika suala hilo kufikia 14,664. Awali makontena 349 yaligundulika kupitishwa kinyemela baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara bandarini na mengine 2,431 kubainika baadaye.
Mbarawa aliwataka mawakala wa forodha na kampuni hizo 283 zinazotuhumiwa katika utoaji wa makotena na magari bila kulipia ushuru kupeleka vielelezo vya uthibitisho ndani ya siku saba kuanzia juzi.
Msemaji wa CCT, Mchungaji John Kamoyo alisema watafanya kama lilivyoagiza kwenda kuchukua barua zao.
“Kama walivyoeleza sisi tutaenda kuchukua barua na kufahamu kilichopo ndani na tutafanya kama walivyoagiza,” alisema Kamoyo huku akikataa kuhusisha wito huo na suala lolote linalohusina na ukwepaji wa kodi.
Katibu mtendaji wa Caritas Tanzania, Laurent Masui alisema atashirikiana na mamlaka hiyo kutimiza agizo hilo.
“Ni kweli tunahusika na utoaji mizigo bandarini lakini kwa wateja mahususi kutoka mashirika ya kidini ambayo husamehewa baadhi ya kodi na ushuru. Lakini tozo nyingine huwa tunalipa na kwa kuwa tangazo lenyewe linaonekana ni la kiutawala, basi nitawatuma maofisa wangu haraka wafuatilie ili tujue kama tulizidisha ushuru au tulitoa pungufu,” alisema Nasui.
0 maoni:
Post a Comment