Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, amewakumbusha wananchi pamoja na taasisi mbalimbali kuendelea kuunga mkono zoezi la uchangiaji wa madawati.
Mkuu huyo wa mkoa, ametoa wito huo jijini Dar es es Salaam wakati akipokea hundi tatu zenye jumla ya shilingi milioni 31. 7 kutoka katika taasisi tatu tofauti.
Wadau hao kutoka katika taasisi hizo za mamlaka ya chakula na dawa TFDA, chuo cha elimu na biashara CBE, na taasisi ya African Relief organisation walikabidhi hundi za fedha hizo ikiwa ni mchango kwaajili ya ununuzi wa madawati katika mkoa wa Dar es salaam.
Kaimu Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) Dk. Emmanuel Munishi (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda (kushoto) Mfano wa hundi ya shilingi milioni 8,000,000/= zilizotolewa na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) kama mchango wa chuo hicho kwa jamii kwa ajili ya kununulia madawati yatakayotumiwa na wanafunzi wa shule za msingi katika mkoa huo.Katikati ni Afisa Uhusiano wa Jamii wa Chuo hicho Leonidas Tibanga.
Wadau hao walitoa wito kwa jamii kuendelea kuchangia madawati bila kuchoka.
Mkurugenzi mkuu mamlaka ya Chakula na dawa TFDA, Hiiti Sillo alisema, “Niseme tu kwamba kazi za TFDA ni kazi za kitaalam , tunatumia vijana waliosoma vizuri kuanzia shule ya msingi kwahiyo tunaamini kama watasoma vizuri katika shule ya msingi na kusoma katika mazingira mazuri basi watakuja kuwa wataalam wazuri katika masuala ya madawa,usalama wa chakula na vipodozi”, alisema.
Kwa upande wake Kaimu msaidizi chuo cha biashara CBE, Emmanuel Munishi, alisema, “Waige mfano wetu kwasababu kule ndiko tunakopata wanafunzi bora kwa maana kule shule za primary tuweze kusupport shule za primary ili waweze kusoma mahali pazuri na tupate wanafunzi wazuri katika vyuo vyetu.”
Pia mwenyekiti wa taasisi ya Kidini na masuala ya kijamii ya African Relief Organisation Sheikh Abdallah Ndauga alisema, “Nataka nishauri umma kwa ujumla hata kwa mtu mmoja kuja kuchangia hata dawati moja moja ili tuweze kusaidia watoto kusoma kwa raha, walau mtu uchangie tu deski moja tu ili tuweze kufika mbali katika suala hili.”
Kwa upande wake Makonda alisema, “Kwa namna moja au nyingine wote hawa wameitikia juhudi za mheshimiwa Rais Magufuli, najua akiona habari hizi Rais anafurahi na kuona ndoto za wanafunzi kusoma bure zinatimia.”
0 maoni:
Post a Comment