Na Yohana Emmanuel
Waziri Mkuu ambaye yuko katika ziara ya
kutembelea nchi za Falme za Kiarabu, ikiwa ni sehemu ya kudumisha ushirikiano
na kutafuta wawekezaji, amekatisha ziara hiyo siku mbili baada ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kujiuzulu kutokana na kashfa ya
Escrow.
Werema alijiuzulu juzi na Rais Kikwete
akaridhia hatua hiyo, huku umma
ukisubiri hatua zaidi dhidi ya mawaziri na watendaji wa Serikali waliotajwa
katika sakata hilo.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Jaji Werema
alisema ushauri wake wa kisheria kuhusu Akaunti ya Tegeta Escrow haukueleweka
na hivyo kuchafua hali ya hewa.
Kwa mujibu wa ratiba ya ziara hiyo, leo Waziri
Mkuu alitarajiwa kufanya mazungumzo na washiriki wa maonyesho ya B2B pamoja na
kutembelea maeneo mengine lakini ziara hiyo imefutwa na badala yake anaondoka
asubuhi kurudi nyumbani.
Baadaye leo Pinda alitakiwa kwenda Doha, Qatar
kwa ziara kama hiyo hadi Desemba 23.
Baada ya kukamilisha jukumu aliloitiwa, Waziri
Mkuu anatarajiwa kurejea Falme za Kiarabu Jumamosi kuendelea na ziara yake.
Chadema yakerwa JK kumsifia Werema
Jana, Chadema kilielezea kusikitishwa kwake na
sifa alizotoa Rais Kikwete kwa Jaji Werema kuwa ni mwaminifu na mwadilifu
wakati amejiuzulu kutokana na kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow.
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), John
Mnyika alisema kitendo cha Rais kumsifu Jaji Werema kinawakatisha tamaa
Watanzania.
“Hakupaswa kupongezwa badala yake Rais
angemwambia kwamba alikuwa kwenye taratibu za kumfukuza kazi,” alisema Mnyika
na kuongeza kuwa hata watuhumiwa wengine katika kashfa hiyo wanaposikia Rais
akimpongeza mwenzao wanaona makosa yao ni jambo la kawaida linaloweza
kupongezwa.
“Hata vyombo vya dola vitaogopa kumshtaki
Werema kwa sababu amepongezwa na Rais kwamba ni mtumishi ambaye alikuwa
mwaminifu na mwadilifu,” alisema Mnyika.
Alisema Watanzania wanasubiri Rais kuwafukuza
kazi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, katibu mkuu wake,
Eliakimu Maswi, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
na bodi nzima ya Tanesco.
“Baada ya kufukuzwa wanatakiwa kushtakiwa,”
alisema Mnyika.
0 maoni:
Post a Comment