Jeshi la Polisi mkoani Singida, linamshikilia
Nawaridi Saidi (45), mkazi wa Dar es Salaam kwa tuhuma za kumtupa mjukuu wake
Mayasa Meshack (6) kutoka ndani ya gari wakati akisafiri kwenda Kigoma akitokea
Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Thobias
Sedoyeka alisema kuwa tukio hilo lilitokea Desemba 18, saa 2 usiku katika
Kijiji cha Igugumo, wilayani Iramba ambapo mama huyo akiwa kwenye basi aina ya
Scania, alifungua dirisha kutoka katika kiti alichokaa na kumtupa Mayasa wakati
basi likiwa katika mwendo.
“Mama alikuwa anaenda mkoani Kigoma kwa ajili
ya Sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya, aliambatana na mtoto wake mwingine
ambaye jina bado halijafahamika,” alisema Kamanda Sedoyeka.
Aliongeza: “Baada ya kumtupa mtoto huyo,
abiria wenzake walianza kupiga kelele, zilizomuamuru dereva kusimamisha basi na
kulirudisha nyuma ili kwenda kumwokota mtoto huyo ambaye alikuwa bado hai.”
Alipelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya
Mkoa Singida na kupokewa na Dk Adam Hussein ambaye alianza kumtibia kwa kuanza
kumtoa uchafu kwenye mfumo wa kupumulia.
“Dk Hussein alimwongezea damu na kumshona
majeraha, hata hivyo saa 2 asubuhi ya Desemba 19, Mayasa alifariki dunia,”
alisema Kamanda Sedoyeka.
Alibainisha kuwa walimpeleka hospitali mama
aliyetupa mtoto huyo kwa ajili ya kumpima akili baada ya kufanya mahojiano ya
awali na baadaye atafikishwa mahakamani.
Kamanda huyo alisema kwamba katika maelezo
yake, mama huyo alisema ana tatizo la kuumwa kichwa na kupoteza kumbukumbu mara
kwa mara, hivyo hakumbuki kama alitenda kosa la kumtupa mtoto huyo, lakini
alishtuka baada ya kupigwa na abiria waliokuwamo kwenye basi hilo.
Awali, mmoja wa abiria waliokuwamo kwenye basi
hilo, Ebenezer Hans alisema kwamba mama huyo akiwa miongoni mwa abiria, alikuwa
na mtoto wake mwenye umri unaokadiriwa miaka 14 na wajukuu wawili, ambao
alikuwa akisafiri pamoja nao.
Alisema abiria waliokuwa jirani naye
walishtuka kufuatia mmoja wa abiria kupiga kelele, baada ya kushuhudia mama
huyo akifungua kioo cha dirisha taratibu na kumtupa mtoto huyo kimyakimya,
wakati gari likiwa kwenye mwendo wa kasi katika eneo hilo lenye mapori mengi.
0 maoni:
Post a Comment