MBUNGE ANDREW CHENGE ANUSURIKA KUPIGWA

 ANUSURIKA KUPIGWA MAWE NA MAKAMANDA WA CHADEMA,MUZIKI MNENE WA CCM WATAJWA KUCHANGIA

 

       Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mbunge wa Bariadi Mgaharibi  mkoani Simiyu Andrew  Chenge (CCM)amenusurika kipigo kutoka kwa wafuasi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mkoani Simiyu baada ya kupita katika ofisi zao akitoka kwenye mkutano wake.

Tukio hilo lilitokea jana majira ya saa moja na nusu usiku baada ya vyama hivyo  CCM na Chadema kumaliza mikutano yao ya hadhara iliyokuwa ikifanyika katika maeneo tofauti mjini Bariadi hali ambayo ilisababisha kuwepo kwa vurugu hizo.

Hali ya hewa ilibadilika baada ya wafuasi wa CHADEMA kuzuia msafara wa Mbunge  huyo na kuanza kurushia mawe magari yaliyokuwa katika msafara huo ambapo mmoja wa makada wake alijulikana kwa jina la Ahmed Ismail alilazimika kurusha risasi tatu hewani ili kuwatawanya watu waliokuwa wameziba njia.



"Hali hiyo imetokea baada ya msafara wa Chenge kuondoka katika mkutano wao uliokuwa katika kijiji cha Isanga jimboni kwake, ambapo wakati wakipita katika ofisi za Chadema Mkoa zilizoko barabara kuu ya Bariadi-Shinyanga walianza kuzomewa na wafuasi wa CHADEMA",walieleza mashuhuda wa tukio hilo.


Akidhibitisha kuwepo kwa tukio hilo Kamishena Msaidizi wa jeshi la polisi Mkoani Simiyu Gemini Mushi alisema kuwa vyama hivyo baada ya kumaliza mikutano yao Chadema walianza safari ya kuelekea katika ofisi zao huku msafara wa  mbunge ulikuwa ukirejea .

Kamanda alibainisha kuwa baada ya msafara huo kufika katika eneo la ofisi ya Chadema walikuta kundi kubwa la watu wakishangilia na ndipo mbunge huyo akashuka kwenye gari na kuanza kucheza nao wakati wakiendelea kushangilia walisikia sauti ikisema rusha mawe hali ambayo ilisababisha mbunge huyo kukimbilia kwenye gari.

Mushi alisema kuwa baada ya wafuasi hao wa Chadema kurusha mawe wakishambulia gari alilokuwa amepanda mbunge huyo, ndipo risasi tatu zilirushwa hewani kwa ajili ya kuwatawanya na kufanikisha wafuasi hao kukimbia na kUtawanyika.

Mushi alieleza kuwa baada ya tukio hilo wafuasi wote wa vyama viwili walikimbilia kituo cha polisi Bariadi kutoa taarifa, ndipo askari wake walifika eneo la tukio na kuanza uchunguzi.

Alisema risasi hizo zilizorushwa na mfuasi huyo wa Chenge zilikuwa na lengo la kuwatawanya wafuasi hao ambao alisema walianza kuleta vurugu, huku akieleza kuwa siLaha hiyo ni bunduki aina ya bastola.

Kamanda huyo alieleza kuwa uchunguzi bado unaendelea kufanyika ili kubaini chanzo cha vurugu hizo, huku akieleza kuwa hakuna majeruhi na hakuna mtu anayeshikiliwa na jeshi hilo.

Mashududa wa tukio hilo

Baadhi ya mashuda wa tukio hilo wameeleza kuwa baada ya kukutana hapo wafuasi wa vyama hivyo waliaza kurushiana mawe na ndipo mbunge kukimbilia kwenye gari na baadhi ya wafuasi wa Chadema walianza kuirushia mawe gari aliyokuwa amepanda mbunge hali ambayo iliwalazimu kurusha risasi mmoja wa makada wa CCM waliokuwa katika gari hilo.

“Tulishangaa kuona wafuasi wa CCM na Chadema kuanza kushambuliana kwa mawe baada ya watu wa CCM kutokea katika mikutano yao ya hadhara na kufika katika maeneo ya Salunda wafuasi wa ccm na Chadema walikutana na kuanza kushambuliana kwa mawe baadaye tulisikia risasi zinalia”Alisema Nkuba Majaliwa shuhuda wa tukio hilo.

Heche asimulia.

Kiongozi wa chama cha Demokrasia na Maendeleo Chadema John Heche alisema kuwa chama cha CCM walipita katika ofisi za chadema wakakuta viongozi wanafanya mikutano ya ndani ambapo msafara wa CCM ulifika katika ofisi hiyo na kuanza kupiga muziki hali ambayo ilipelekea baadhi ya viongozi kutoka kwenda kuwazuia kwa madai ya kupunguza muziki.

“Msafara wa CCM ulifika katika ofisi ya Chadema baada ya kutoka katika mikutano yao walipofika katika maeneo ya ofisi zetu walisimamisha magari yao na kuanza kupiga muziki na wafuasi wao waliteremka kwenye magari na kuanza kucheza hali ambayo tulienda kuwazuia kwa misingi ya kupunguza muziki kwani tulikuwa tunafanya kikao cha chama lakini walikaidi na ndipo wafuasi wetu walianza kuwashambulia kwa mawe hali ,wao walirusha risasi hewani kwa ajili ya kutawanya”Alisema Heche.

Kwa upande wake katibu wa umoja wa vijana wa CCM wilaya ya Bariadi Sai Samba alieleza kuwa baada ya kufika katika eneo la ofisi ya Chadema walikuta kundi kubwa la vijana wakiwa barabarani ambapo walipofika wakazuia msafara na ndipo kundi la vijana walianza kumrushia mawe mbunge wao. 

Alisema baada ya kuona hali hiyo mmoja wa makada wao aliamua kurusha risasi hewani ili wafuasi hao wasimdhuru Mbunge huyo ambaye gari lake lilikuwa likishambuliwa kwa mawe.

“Baada ya kufika katika maeneo ya ofisi ya Chadema tulikuta watu       ambao walikuwa wamejiandaa kwa ajili ya kuushambulia msafara wa mbunge Andrew Chenge na tulipofika pale walianza kucheza na mbunge akateremka kwenye gari na kuanza kucheza nao lakini ilisikika sauti ikiamuru vijana kurusha mawe na ndipo walianza kurusha mawe hali iliyopelekea kurusha risasi hewani”,alisema Samba


Walipotafutwa kuongelea suala hilo la kurusha risasi hewani Mbunge wa Bariadi Magharibi na kada huyo wa CCM Ahmed Ismail hawakupokea simu lakini baadaye mbunge huyo alisema hawezi kuzungumzia suala hilo bali jeshi la polisi ndilo linaweza kuzungumzia suala hilo.

0 maoni:

Post a Comment