Blatter agoma kujiuzulu :Platini
Rais wa shirikisho la soka Duniani FIFA Sepp Blatter,amekataa kata kata kujiuzulu.
Rais wa shirikisho la soka barani ulaya Michel Platini amewambia waandishi wa habari kuwa Blatter amekataa wito wa kujiuzulu.
Platini amesema kuwa kufuatia uamuzi huo UEFA sasa itashiriki uchaguzi hapo kesho na imewashauri washirika wake kumpigia kura mpinzani wa Blatter mwanamfalme Ali bin al-Hussein kutoka Jordan.
Bara la Afrika limeahidi kumpigia kura Blatter sawa na shirikisho la bara Asia.
Blatter mwenye umri wa miaka 79 anawania nafasi ya kuwa rais wa FIFA kwa kipindi cha tano mfululizo.
Viongozi kadhaa walikuwa wamependekeza kuhairishwa kwa uchaguzi huo huku wengine wakimtaka ajiuzulu ilikuwepo na mwanzo mpya katika FIFA.
Awali ,Blatter aliongoza kikao cha dharura cha wanakamati wakuu wa shirikisho hilo huko Zurich Uswisi.
Kikao hicho kinafuatia hatua ya kukamatwa kwa maafisa 7 wakuu na polisi huko Zurich Uswisi kwa tuhuma za ufisadi.
Blatter anakabiliwa na shinikizo la kujiuzulu uongozi wa FIFA.
Hata hivyo FIFA inasema kuwa kura za kumchagua rais mpya zilizoratibiwa kufanyika kesho zitaendelea mbele.
FIFA ilijipata katika mkono mbaya wa sheria baada ya maafisa wa kitengo cha FBI kupendekeza kushtakiwa kwa maafisa wakuu 14 wa shirikisho la soka duniani FIFA kwa tuhuma za ulaji rushwa na ufisadi.
Aidha mdhamini mkuu wa FIFA kampuni ya VISA sasa imeonya kuwa huenda ikalazimika kutathmini upya uhusiano baina yake na FIFA hususan kufuatia kukamatwa kwa maafisa 7 Zurich Uswisi kwa madai ya ufisadi.
Wadhamini wengine McDonald's, Adidas na kampuni ya kutengeza magari ya Hyundai wamesema kuwa wanafuatilia kwa karibu sana matukio katika shirikisho hilo.
Coca-Cola, kwa upande wake imesema kuwa matukio hayo yameathiri kwa kiwango kikubwa mno hadhi ya mashindano ya kombe la dunia.
Hatua hiyo inafanyika baada ya kukamatwa kwa viongozi wakuu wa shirikisho hilo hapo jana Jumatano kwa madai ya ulaji rushwa na ubadhirifu wa fedha.
Makampuni hayo ambayo hutoa mamilioni ya dola katika ufadhili ilikushirikishwa katika mashindano ya FIFA yanatazama kwa makini mikakati inayoendelea ya kupambana na ufisadi ndani ya shirikisho la soka duniani FIFA.
0 maoni:
Post a Comment