UKOSEFU WA UMEME NIGERIA NI TATIZO KWA WANAFUNZI NCHINI HUMO...
Tatizo kubwa la ukosefu wa nishati ya umeme na fueli nchini Nigeria limewafanya wanafunzi walazimike kudurusu masomo yao kwa kutumia umeme wa taa za barabarani ili kuweza kujiandaa na mitihani yao.
Kukauka kwa vituo vya petroli na kukatwa umeme katika maeneo mengi kumewafanya wanafunzi ambao hakuna umeme majumbani kwao wala madarasani mwao walazimike kudurusu masomo yao katika mazingira yasiyo ya kawaida.
Wakati huu ambapo wanafunzi wanajiandaa na mitihani ya mwisho wa mwaka wa masomo, baadhi ya wanafunzi wanaonekana wakidurusu masomo wakati wa usiku kwenye barabara kuu kwa kutumia umeme unaowaka kwenye taa za nguzo za barabarani.
Walimu wameeleza kuwa ufaulu wa wanafunzi unaporomoka pamoja na kiwango cha ubora wa sekta nzima ya elimu nchini Nigeria.
Nchi hiyo ambayo ni mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta barani Afrika hivi sasa inaagiza kutoka nje karibu kiwango chote cha mafuta ya petroli yaliyosafishwa inayoyahitajia kwa ajili ya matumizi ya ndani.
Serikali inalaumu hujuma zinazofanywa kwenye mabomba ya mafuta na gesi pamoja na migomo ya wafanyakazi wa sekta ya mafuta kuwa ndio chanzo cha hali mbaya ya uhaba wa nishati za umeme na mafuta unaoshuhudiwa hivi sasa nchini humo.
Uhaba mkubwa wa petroli na dizeli katika maeneo mengi zikiwemo hospitali unakwamisha utoaji huduma mbalimbali. Serikali mpya ya Nigeria itakayoongozwa na Rais mteule Muhammadu Buhari inatazamiwa kuapishwa hivi karibuni. Changamoto kadhaa zitaikabili serikali hiyo zikiwemo za ufisadi, hali mbaya ya usalama, uchakavu wa miundombinu na huu wa sasa wa tatizo la uhaba wa nishati
0 maoni:
Post a Comment