Makongoro Nyerere akitangaza nia ya kugombea urais wakati wa mkutano ulifanyika katika Kijiji cha Mwitongo, Butiama mkoani Mara jana. Picha na Peter Saramba
Mtoto wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Charles Makongoro, ametangaza nia ya kuwania urais, akisema anaomba kibali kuisaidia CCM iache rushwa, kuparaganyika na atakapoingia madarakani, ili asiwaangushe Watanzania, anahitaji chama imara kisicho na shaka kama ilivyo sasa.
Akitangaza nia hiyo nyumbani kwao Mwitongo, Butiama jana, Makongoro alisema kutokana na CCM “kubakwa na vibaka,” inawavunja moyo wanachama na inawakatisha tamaa Watanzania, hivyo inahitaji kiongozi anayewarudishia matumaini.
“Sisi ndiyo wazalendo tunasema mnapotaka kutupora hiki chama sisi tupo, turudishieni na mnapoturudishia kipitishie kwa Makongoro Nyerere mna uhakika chama hiki hakipotei siyo kumkabidhi kibaka,” alisema Makongoro.
Kabla ya kutangaza nia hiyo alisema, “nitangaze nisitangaze?, Nitangaze nisitangaze,” akajibiwa na watu waliohudhuria hafla hiyo ‘tangazaaa...’.
Makongoro aliyesema Sh1 milioni za kuchukulia fomu anazo hivyo haitaji kuchangiwa, alikataa kusoma hotuba iliyoandaliwa kwa ajili ya kutaja vipaumbele vyake atakapoingia madarakani na kuwashangaa wenzake waliotangaza nia kwa kutaja vipaumbele, kuwa wanafanya faulo kwa sababu ilani ya chama haijatoka.
Alisema wametangaziwa na chama kuwa ilani itakuwa tayari Julai na kwamba hawezi kutoa kipaumbele vyake halafu baadaye vitofautiane na vitakavyobainishwa na chama ili asije kulaumiwa.
“Nipo hapa kukiri kwamba sehemu kubwa ya tatizo la CCM ni kutofuata utaratibu, ukiona kuna kazi inaombwa kwa kufuata utaratibu na wanaoomba hawafuati utaratibu hawa washtukie mapema, hawafai,” alisema Makongoro na kuongeza:
“Ukiona mtu anayeomba kazi na hafuati utaratibu huo ilhali akiujua, ujue siku ukimpa kazi biashara ya kwanza akifika pale ni kufuta utaratibu huo na kuweka wa kwake ili akae mpaka awe mfalme wa nchi hii, usimpe!”
Makongoro alisema kibaya zaidi viongozi wa CCM ambao wameshiriki kuweka utaratibu huo ndiyo wanahusika na kwamba, ingawa kikao chake hakikuwa cha kuwataja kwa majina walioshiriki kuvunja utaratibu huo lakini hana jinsi lazima awataje.
Aliwataja baadhi ya wagombea waliokwishatangaza nia ndani ya chama hicho akisema wamekiuka utaratibu kwa kutoa ahadi wakati ilani ya chama hao haijapitishwa na mkutano mkuu.
“Wewe (anamtaja mgombea) ni mjumbe wa NEC umeshiriki na unajua kuwa rasimu ya ilani itapitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM, wewe unatangulia kimbelembele, nakuuliza wewe nani?”
Makongoro alimpiga kijembe mgombea mwingine akisema hana wasiwasi na uadilifu wala uwezo wa kiongozi huyo lakini hazingatii msamiati wa kung’atuka kwa kuwa amekuwapo ndani ya Serikali kwa muda mrefu.
Kijembe kwa Rais Kikwete
Kuhusu mtifuano miongoni mwa wanaCCM na tuhuma za ufisadi dhidi a viongozi wa chama na Serikali, Makongoro alisema yote hayo yanatokana na kosa la Rais Kikwete kuwapenda isivyo kifani marafiki zake ambao huishia kumvunjia heshima.
“Kosa la Rais Kikwete ni kuwapenda sana marafiki zake. Kwa bahati mbaya baadhi ya marafiki zake hao ni vibaka. Kibaka ni kibaka tu hata akipewa gari la Serikali na kupeperusha bendera ya Tanzania, bado ataendelea kuwa kibaka tu,” alisema Makongoro bila kutaja majina.
Alisema haoni haya kukiri kuwa wamo vibaka ndani ya CCM kwa sababu hata vyama vya upinzani navyo vina vibaka wao.
“Ni kujidanganya kusema hakuna vibaka ndani ya CCM wakati wapo na wanatumia fedha zao, nyingine walizopata kwa wizi kukivuruga chama,” alisisitiza Makongoro.
Kuhamia upinzani 1995
Akizungumzia uamuzi wake wa kuhamia upinzani mwaka 1995 alikogombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini na kushinda kupitia Chama cha NCCR – Mageuzi, Makongoro alisema mizengwe, rushwa na chama kugeuzwa kuwa cha matajiri na wenye fedha ndicho kilichomkimbiza na alipata baraka zote kutoka kwa baba yake Mwalimu Nyerere.
“Watu wataanza kusema kuhusu mimi kuhamia upinzani na baadhi eti wanadai nina laana ya kukihama chama alichoasisi baba yangu. Hivi kweli mie naonekana kama mtu mwenye laana? Hivi naonekana kama mtu mlevi mimi?” alisema na kuhoji Makongoro na kuongeza:
“Mizengwe kwenye kura za maoni ndani ya CCM na matumizi ya fedha kununua uongozi ndivyo vilinifanya kuhamia upinzani baada ya wazee waadilifu ndani ya CCM kunishauri nihame ili wanipe fursa ya kutumikia wananchi wa Arusha kupitia nafasi ya ubunge,” alisema Makongoro.
Alisema baada ya kutangaza nia kugombea ubunge wa Arusha Mjini mwaka 1995, huku akitiwa moyo na wazee na wanachama wengi, alijikuta akikimbiwa na viongozi wote wa chama kila alipofanya ziara ya kujinadi katika kata zote 17 za jimbo hilo wakati huo.
“Walionishauri kutoka CCM kwenda NCCR-Mageuzi ni wazee na waasisi wa CCM. Kabla ya kuhamia upinzani, nilimwarifu Mwalimu Nyerere na kupata baraka zake zote,” alisisitiza Makongoro.
Alisema ingawa alipanga kuhamia upinzani bila kumweleza Mwalimu Nyerere, mke wake, Jaji Aisha Nyerere ndiye aliyeshurutisha kupata kwanza baraka za mwasisi huyo wa Taifa ikabidi yeye na mkewe wafunge safari hadi Dodoma kumtaarifu Mwalimu Nyerere uamuzi huo huku akiwa na hofu ya kutopokewa wazo lake, ingawa matokeo yalikuwa kinyume na hofu yake.
“Nilihama CCM kwenda upinzani siyo kwa kupenda, bali nililazimishwa,” alisema.
Maradhi ya CCM
Alisema: “CCM kinaugua maradhi ya kukaa madarakani kwa muda mrefu na dalili za maradhi hayo ni kuteua wagombea bila kujali matakwa ya wananchi.”
Alitaja dalili nyingine kuwa ni viongozi wa CCM kuzungumza maneno yasiyolingana na matendo yao.
“CCM iongoze kwa matendo badala ya maneno. Chama kinanuka rushwa. Taifa linanuka rushwa. CCM ichukue hatua na kutokomeza rushwa na ufisadi unaotishia kuangamiza taifa letu.
“Nikipata ruhusa ya chama changu na kibali cha wananchi, nitaanza safari ya kuwaambia vibaka turudishieni chama chetu. CCM ni chama cha wakulima na wafanyakazi, waturudishie chama chetu.”
Kununua nyumba Ulaya, Dubai
“Wapo waliotangaza nia ambao wanajinasibu kununua nyuma Dubai na sehemu kadhaa huko Ulaya na kwingineko. Wasijidanganye kwa sababu wakiharibu huku na kukimbilia huko watambue watakuwa wakimbizi tu. Hapa ndipo petu sote,” alisema.
Alisema hata utajiri wanatuambia hivi sasa wameupata wakiwa ndani ya CCM kwa sababu baadhi yao walikuwa maskini walipojiunga na utumishi wa chama cha Serikali.
“Fedha zote, nyingine halali na nyingine haramu wamezipata ndani ya CCM. Sasa hawa waliotajirika kwa kuwamo ndani ya CCM wanataka kukipore chama hiki kutoka mikononi mwa wananchi walio wengi. Haiwezekani waturejeshee chama chetu,” alisema Makongoro.
Makundi ndani ya CCM
Akizungumzia makundi ndani ya CCM, hasa nyakati za uchaguzi, Makongoro alisema anayachukia makundi ya siku hizi kwa sababu yanakivunja chama kutokana na wahusika kutoyavunja uchaguzi unapomalizika.
“CCM hivi sasa ina makundi. Kila mgombea ana timu yake na msingi mkuu wa timu hizi ni fedha na wanaojiunga nayo wanafuata fedha. Leo hii nikiwa na hela hata walioko kwa wagombea wengine wananifuata.
“Binafsi sina kundi na ninayachukia sana haya makundi kwa sababu yanakivuruga chama chetu. Wenye fedha wageuka wafugaji wa watu badala ya mifugo. Yaani wenye fedha siku hizi wanamiliki watu wakiwamo wajumbe wa halmashauri kuu. Haiwezekani,” alisema Makongoro
Mkono yuko na Makongoro
Miongoni mwa waliohudhuria hafla hiyo ni Mbunge wa Musoma Vijijini, Nimrod Mkono ambaye alisema watia nia waliokuwa wanamfuata ili awaunge mkono kuanzia sasa “bye bye”, watambue yupo na Makongoro Nyerere.
Mkono alisema wapo wengi waliokuwa wakitaka kujua aliopo kati ya watia nia ya urais, “Mmesikia mengi, Simba wa Butiama amekohoa hakuna mwingine. Makongoro ndiye aliyenifanya mimi kuwa mbunge, amenitembeza kijiji kwa kijiji mngenishangaa kusikia niko kundi jingine,” alisema Mkono na kuongeza:
“Nitajitolea kwa hali na mali, nitamtembeza Makongoro nchi nzima, wale waliokuja kwangu bye bye niko kwa Makongoro.”
Alisema Makongoro ni miongoni mwa vijana waliolelewa katika maadili ya itikadi za uongozi na pia ametoka katika jiko la viongozi wa ngazi kubwa tangu ukoloni.
Mkono alisema Makongoro akiongoza nchi, kuna uhakika wa kuwa katika mstari mmoja mnyoofu kwani hana hofu yoyote kwa Watanzania katika kuendesha gurudumu la maendeleo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Rorya, Samwel Kiboye alisema Watanzania kumuenzi Baba wa Taifa kwa kuadhimisha sikukuu haitoshi, bali wafanye hivyo kwa kumkabidhi kijana wake Makongoro fimbo ya kuwaongoza.
“Tukimkabidhi kijana wa Baba wa Taifa viatu vya baba yake tutakuwa tumemuenzi kiuhakika Baba wa Taifa hili, kwanza kijana huyu ni mwadilifu na pia ni kiongozi shupavu kwani mifano yake tunayo na tulishaionja wakati akiwa mwenyekiti wa mkoa huu,” alisema Kiboye.
Kiboye alisema Makongoro ni kati ya viongozi ambao hawana harufu ya ufisadi, ubadhilifu wa aina yoyote wala si mla rushwa hivyo endapo atapewa nafasi ataongoza katika misingi ya kuleta mafanikio na kuondokana na kero zinazochangia kuondoa uzalendo wa nchi.
Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shy – Rose Bhanji alisema anaamini Makongoro ndiye kiongozi anayetakiwa kuvaa viatu vya Baba wa Taifa kulingana na sifa alizonazo katika utendaji wake wa kazi katika nafasi alizowahi kushika na aliyopo hivi sasa ya ubunge wa Afrika Mashariki.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Butiama, Yohana Mirumbe alisema wanachama wa wilaya hiyo kwa pamoja wako tayari kumuunga mkono Makongoro katika kugombea nafasi ya kuwa mgombea wa CCM katika nafasi ya urais.
Mirumbe alisema lengo ni kutaka kiongozi atakayeweza kumalizia kazi itakayoachwa na rais aliyepo madarakani ya kuongoza nchi na kuiweka katika hali ya kusaidia wananchi kuondokana na hali ngumu ya maisha.
Apewa kifimbo
Mwenyekiti wa ukoo wa Burito ambaye pia ni Chifu wa Kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi alisema Makongoro kutangaza nia hakukosea, bali ni historia ya ukoo aliotoka kuwa na karama za kuongoza tangu enzi za ukoloni kabla ya uongozi wa kisiasa.
Chifu Wanzagi alimkabidhi kifimbo Makongoro akitaka Watanzania kumsikiliza na kumwelewa.
“Ukoo huu umekuwa ukitoa viongozi na kuaminiwa na jamii. Makongoro anatoka ukoo wa kichifu, ukoo huu hata siku moja haufanyi kitu kwa kubahatisha au kujaribu,” alisema Chifu Wanzagi na kuongeza:
“Kama tungekuwa na shaka na Makongoro, tusingekubali asimame, kwa sababu angetushushia heshima kwa jamii, Watanzania, Afrika na Dunia.”
0 maoni:
Post a Comment