Bunge limesikia maoni ya wadau ya kuuondoa Bungeni Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari 2015 ambao ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya pili Juni 27, mwaka huu.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alithibitisha hayo jana kwenye viwanja vya Bunge wakati akihojiwa kutaka kujua iwapo ushauri wa kamati umemfikia Spika na uamuzi juu ya suala hilo.
“Ushauri wa kamati umezingatiwa, Muswada umeondolewa Bungeni,” Dk. Kashilillah.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, alisisitiza kuwa maoni ya wadau hayawezi kupuuzwa katika uandaaji wa Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2015.
“Hatutapuuza maoni ya wadau hasa yanayolenga kuboresha muswada husika. Utungaji wa sheria yoyote ni lazima uwe shirikishi, hivyo maoni ya wadau yamesikikizwa kama ilivyokuwa awali walishauri Muswada huo na ule wa Huduma kwa Vyombo vya Habari, usije kwa hati ya dharura, tulizingatia na uliondolewa,”alibainisha.
Juni 22, mwaka huu, wadau mbalimbali wa habari waliokutana jijini Dar es Salaam, walipinga miswada hiyo kwa kile kinachoelezwa kuwa inakiuka sheria za kimataifa, Katiba ya nchi na kuwanyima haki raia kupata taarifa na kuua ndoto ya vijana wanaotarajia kunufaika na tasnia ya habari.
Wadau hao ni Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania ( MOAT), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISA) Tawi la Tanzania na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu ( THRDC).
Mmiliki wa Kampuni ya New Habari Corperation, Rostam Aziz, alisema muswada huo ni mbaya kwani unazuia dhana nzima ya uwazi na ukweli hivyo kulirudisha taifa nyuma na kuitaka serikali kutopeleka bungeni hadi wadau wote wa tasnia ya habari watakapotoa maoni.
“Serikali isifanye haraka, muswada huu utaturudisha nyuma kama taifa. Usitishwe kupelekwa bungeni hadi pale wadau wote watakapotoa maoni yao,” Rostam.
Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema baraza hilo limetoa ombi hilo kwa sababu wadau wa habari hawakuwa na muda wa kutosha kutoa maoni yao baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita.
0 maoni:
Post a Comment