Jaji mmoja katika jimbo la Louisiana nchini Marekani ameamuru kuachiliwa huru kwa mfungwa ambaye amekuwa akizuiliwa bila kupewa ruhusa ya kutangamana na watu wengine kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40. Jaji James Brady kadhalika amewapiga marufuku viongozi wa mashtaka kumfungulia tena mashtaka kwa mara ya tatu Albert Woodfox, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 68.
Amekuwa kizuizini bila kuruhusiwa kuonana na mtu yeyote tangu tarehe 18 mwezi Aprili mwaka 1972 kufuatia vurugu za gerezani ambazo zilisababisha kifo cha askari jela mmoja.
Woodfox alifunguliwa mashtaka na kesi yake kusikilizwa mara mbili lakini mashtaka yote mawili yalitupiliwa mbali baadaye. Anazidi kukanusha mashtaka hayo.
Siku ya jumatatu, Jaji Brady aliamuru Woodfox kuachiliwa huru bila masharti yoyote, na vilevile kuwazuia viongozi wa mashtaka kumfungulia mashtaka menginne akisema haitakuwa haki.
''Angola Three''
Woodfox ni mwanachama wa mwisho wa kundi la wafungwa watatu wanaojulikana kama ''Angola Three''
Wenzake wawili- Robert King na Herman Wallace - waliachiliwa huru mwaka 2001 na 2013 mtawalio.
Wote watatu walijihusisha na harakati za chama cha Black Panther, na wamekuwa wakisisitiza kuwa walifungwa jela kwa makosa ambayo hawakuhusika-hukumu zao zikitolewa baada kesi zilizoendeshwa kiholela.
Walizuiliwa katika mazingira ya upweke katika gereza la jimbo la Louisiana, Louisiana State Penitentiary, ambalo lilibandikwa jina la Angola kutokana na shamba kubwa la mimea ya kilimo lilikojengwa gereza hilo. Wafanyikazi katika shamba hilo walikuwa watumwa kutoka Afrika. Masaibu ya watu hao yamekuwa yakiangaziwa kwa kipindi kirefu na makundi ya kimataifa ya kutetea haki.
0 maoni:
Post a Comment