MADIWANI MKOANI SHINYANGA WATAKIWA KUACHA KUFANYA SIASA ZA KISHAMBA ...



Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro


Madiwani wanaomaliza muda wao wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, wameonywa kutofanya siasa za kuchafuana majukwaani,pale wanapotetea viti vyao vya kupewa ridhaa tena na wananchi ya kuwaongoza kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Josephine Matiro, alisema siasa za kuchafuana zilishapitwa na wakati hivyo madiwani wanapaswa kutoa sera zao na kuwaeleza wananchi yale waliyoyatekeleza, watawachuja kama wanawafaa kuwaongoza kwa mara nyingine na siyo kufanya siasa za kuchafuana.

Akizungumza wakati wa kikao cha kuvunja baraza la madiwani wa manispaa hiyo kilichofanyika juzi katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ,Matiro alisema siasa ya sasa inaonekana kwa vitendo hivyo madiwani na kufanya kazi kubwa kwa wananchi.

“Naombeni sana madiwani pale mlipokwaruzana msameheane, mtakaporudi katika majukwaa ya kuwaomba wananchi ridhaa tena ya kuwaongoza kwa miaka mingine mitano, mfanye siasa kwa amani na utulivu bila ya kuvunja sheria za uchaguzi,” alisema Matiro.


Wakati huo huo mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga ameeleza kuwa uhusiano usioridhisha kati ya watendaji wa serikali na madiwani wa halmashauri ya manispaa ya Shinyanga umesababisha miradi ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa maabara katika shule za sekondari kusuasua. 

Rufunga alisema katika kipindi cha miaka mitano ya baraza hilo,kumekuwa na uhusiano mbovu kati ya watendaji wa serikali na madiwani hali iliyosababisha manispaa hiyo kufanya vibaya katika utekelezaji wa ujenzi wa maabara hali iliyofanya manispaa hiyo iwe ya pili kutoka mwisho kati ya halmashauri sita za mkoa huo. 

“Kulikuwa na hali ya dharau na hali ya madiwani kutotii maagizo yanayotoka serikalini,kitendo kilichosababisha baadhi ya madiwani kuzuia wananchi wasichangie shughuli za maendeleo hususani katika ujenzi wa maabara”,alieleza Rufunga. 

“Katika kutekeleza agizo la rais la ujenzi wa maabara manispaa ya Shinyanga,imefanya vibaya imetekeleza kwa asilimia 40 tu na halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Vijijini asilimia 35,Kishapu asilimia 90,wakati halmashauri za Ushetu,Msalala na Kahama Mji wakiwa wametekeleza kwa asilimia 100”,aliongeza Rufunga. 

Mkuu huyo wa mkoa alisema kulikuwa na msukumo mdogo sana kwa baadhi ya madiwani katika kuhamasisha wananchi kuchangia shughuli za maendeleo hali iliyochangiwa kwa kiasi kikubwa na itikadi za vyama vya siasa. 

“Naomba katika kipindi kijacho,madiwani muepuke itikadi za kisiasa,maendeleo hayajali itikadi za vyama,mkifanya hivi hamuwatendei haki wananchi,leo hii wanafunzi wetu hawana maabara za kujifunzia kwa sababu ya itikadi zenu”,aliongeza Rufunga. 

Katika hatua nyingine Rufunga aliwataka madiwani ambao walitumia nafasi hiyo kufanya utalii badala ya kuwaletea maendeleo wananchi waachane na nafasi hiyo katika uchaguzi ujao kwani wananchi wanahitaji kiongozi mchapakazi badala ya kiongozi mtalii. 

Aidha aliwataka watendaji wa manispaa hiyo na madiwani kuwa wabunifu katika kutafuta vyanzo vya mapato kwani uhai wa halmashauri yoyote unatokana na vyanzo vizuri vya mapato. 

Akifunga baraza la madiwani,mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafidh Mukadam aliwapongeza watendaji wa serikali na madiwani wa manispaa hiyo katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoifanya manispaa hiyo ipate hati safi katika miaka mitano mfululizo. 

Mukadam alisema manispaa ya Shinyanga imeshindwa kufanya vizuri katika ujenzi wa maabara katika shule za sekondari kutokana na kukosa vyanzo vya mapato ingawa imefanya vyema katika ujenzi wa miundo mbinu ya barabara.

Na Marco Maduhu- Malunde1 blog Shinyanga

0 maoni:

Post a Comment