MGOMBEA UBUNGE LUDEWA APIGWA CHINI AANGUKIA PUA NAFASI NEC,ASEMA HATAWEZA KUGOMBEA TENA

MBIO za ubunge jimbo la Ludewa mkoani Njombe zimeishia hewani kwa mtangaza nia wa wanafasi hiyo Injinia Zephania Chaula baada ya kuambilia kura 11 pekee katika nafasi ya mjumbe wa Halmashauri kuu ( NEC) Taifa kutoka wilaya ya Ludewa aliyokuwa akiwania dhidi ya katibu msaidizi wa mbunge wa jimbo la Ludewa Hilaly Nkwera aliyeibuka mshindi kwa kupata kura 138 kati ya kura zote halali 151 zilizopigwa . 

Huku mgombea huyo aliyeshindwa katika nafasi hiyo ya Ujumbe wa NEC Injinia Chaula akiapa kutogombea tena nafasi hiyo kwa madai kuwa ni mara ya pili sasa anashindwa vibaya katika mchakato wa kuwania nafasi hiyo ambapo awali alishindwa mgombea wa darasa la saba marehemu Elizabeth Haule . 

Uchaguzi huo mdogo wa kuziba nafasi ya mjumbe wa NEC iliyoachwa wazi na aliyekuwa mjumbe wa nafasi hiyo Elizabeth Haule aliyefariki dunia mapema mwaka huu,ulifanyika mwishoni mwa wiki hii kwa kuwashirikisha wagombea hao wawili kabla ya mgombea mwingine ambae ni mbunge wa jimbo la Ludewa Deo Filikunjombe kuandika barua ya kujitoa katika kinyang'anyiro hicho akiwapisha wagombea hao wachuane kutokana na yeye kudai kuwa atachukua fomu ya kugombea tena ubunge wa jimbo hilo la Ludewa . 

Akitangaza matokeo hayo ya uchaguzi msimamizi mkuu wa uchaguzi huo Lucas Nyanda ambae ni katibu wa jumuiya ya wazizi wa CCM mkoa wa Njombe ,alisema kuwa jumla ya wajumbe waliopaswa kushiriki katika uchaguzi huo ni 164 ila wajumbe halali walioshiriki ni 151 na kati ya wajumbe hao kura 2 ziliharibika huku Injinia Chaula akipata kura 11 na mshindi wa nafasi hiyo Bw Nkwera akipata kura 138 


Awali mbunge wa jimbo la Ludewa Bw Filikunjombe ambae alikuwa ni mmoja kati ya wana CCM watatu ambao majina yao yalirejeshwa kuwania nafasai hiyo alisema kuwa analazimika kujitoa katika nafasi hiyo ili kupisha wanachama hao wawili ambao wamemzidi umri ili kuweza kupambana na yeye ataendelea kuwa kuwatumikia wananchi wa Ludewa katika nafasiya ubunge pekee. 

Akiwashukuru wajumbe kwa ushindi huo wa nafasi ya ujumbe wa NEC Bw Nkwera ambae kitaaluma ni mwalimu na pia amepata kuwa mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa na mwenyekiti wa madiwani wa mkoa wa Njombe na Iringa alisema kuwa amefurahishwa na imani kubwa ambayo wana CCM wameionyesha kwake kwa kumchagua kuwa mwakilishi wao katika vikao vya kitaifa . 

Bw Nkwera alisema wana CCM Ludewa waamini kuwa nafasi hiyo hawajakosea kumpa na kamwe hatawaangusha kwani atahakikisha anawatumikia vema katika vikao vya juu kwa kuanza na safari ya kumpata mgombea wa nafasi ya Urais wa CCM ambae atakuwa ni chaguo la wana CCM wote wa Ludewa . 

Huku Chaula mbali ya kuwashukuru kwa kura 11 alizopata bado alisema kuwa hatakuwa tayari kuendelea kugombea tena kwani yawezekana kabisa Mungu hajapenda yeye kuwa kiongozi wa kisiasa bali ametaka aendelee kuwa mtaalam .

 “Nasema haya kutoka moyoni mimi ni mwanachama hai wa chama cha mapinduzi na nakipenda chama changu hivyo naahidi sitagombea tena katika maisha yangu nafasi hii ya UNEC kutokana na ukweli kuwa nahisi siasa inanikataa maana kila nikigombea nashindwa hivyo ngoja nifanye kazi nyingine pia nampongeza sana mshindi Mzee Nkwera katika utendaji wake ndani ya chama”,alisema Mhandisi Chaula. 

Wakati huo huo serikali ya mkoa wa Njombe kupitia mkuu wa mkoa wa Njombe Dr Rehema Nchimbi imempongeza kwa kumpa hati ya shukrani mbunge wa jimbo la Ludewa Bw Filikunjombe kwa ushiriki wake mkubwa katika kufanikisha mbio za mwenge katika mkoa huo kwa kuwa mbunge pekee kushiriki mbio za mwenge na kuchangia vizuri . 

Akikabidhi hati hiyo mbele ya wajumbe wa mkutano wa Halmashauri kuu , mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Anatory Choya aliweza kumtunuku hati hiyo ya heshima mbunge wa jimbo la Ludewa Filikunjombe kwa kushiriki kimamirifu katika mbio za mwenge wa Uhuru ndani ya mkoa wa Njombe. 

Akitoa cheti hicho Bw.Choya alisema kuwa kutokana na ushiriki alioufanya mh.Filikunjombe katika mbio cha mwenge wa Uhuru mkuu wa mkoa wa Njombe na ofisi yake wameona wampatie cheti cha heshima Filikunjombe kwani ni mbunge pekee aliyeshiriki katika mbio hizo za Mwenge katika mkoa wa Njombe.

0 maoni:

Post a Comment