Akiwa anaichezea Platinum FC ya Zimbabwe, Donald Ngoma aliifungia timu yake mabao 16 msimu uliopita, lakini hivi sasa akiwa na Yanga amepanga kuongeza kasi ili afunge mabao mengi kuzidi aliyoyapachika akiwa na klabu yake ya zamani.
Ngoma ametua kuichezea timu hiyo hivi karibuni pamoja na Mghana, Joseph Zuttah, kila mmoja akisaini mkataba wa miaka miwili na tayari ameshaifungia Yanga bao moja kwenye mchezo wake wa kwanza klabuni hapo, wa kujipima nguvu dhidi ya KMKM.
Ngoma, raia wa Zimbabwe, amesema anataka kufunga mabao mengi zaidi iwezekanavyo lakini akaomba apewe muda ili azoeane vyema na wenzake.
“Malengo yangu ni kupita idadi ya mabao 16 niliyofunga nikiwa na Platinum kwa kuanzia mechi za ligi kuu na michuano ya kimataifa.
“Ninaamini nitaifikisha na kuipita idadi hiyo ya mabao niliyofunga nikiwa na Platinum na hilo nitafanikiwa kama nitapata ushirikiano mzuri wa wachezaji wangu katika kunipa pasi nzuri,” alisema Ngoma.
0 maoni:
Post a Comment