MSUVA ASEMA MUDA UTAFIKA YEYE KUONDOKA YANGA!!!


Mfungaji bora wa ligi kuu kwa msimu uliopita na kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva, ametamka wazi kuwa yupo huru kutimka muda wowote ule ndani ya kikosi hicho cha Jangwani endapo atapata timu nje ya nchi.


Msuva ambaye pia ni mchezaji bora katika msimu uliopita, wikiendi iliyopita aliongeza mkataba wa kuitumikia timu hiyo kwa miaka miwili zaidi ambapo sasa atadumu katika klabu hiyo mpaka mwaka 2018.

Msuva amesema licha ya kusaini mkataba huo wa miaka miwili, akili yake bado ipo katika kukihama kikosi hicho siku moja na kwenda kucheza soka la kimataifa pale atakapopata timu.

“Nimesaini mkataba wa miaka miwili zaidi ya kuwa hapa Yanga lakini napenda kuwaambia watu kuwa nitaondoka muda wowote ule ndani ya kikosi hiki pale ambapo nitakuwa nimepata timu ya kwenda kuichezea nje ya nchi.

“Na katika mkataba ambao nimeusaini wiki iliyopita, kuna kipengele ambacho kinaniruhusu mimi kuondoka mara moja pale nitakapopata timu nje na hata viongozi wangu wanalitambua jambo hilo, hivyo nitakuwa huru kuondoka muda wowote ule ilimradi timu itakayonitaka iwe tayari kuwalipa Yanga,” alisema Msuva. 


0 maoni:

Post a Comment