UCHAMBUZI WA MAKALA;....HEBU FUATILIA CHAMBUZI HIIN NIMEKULETEA MUDA HUU HAPA KUHUSU SIRI ILIYOPO JUU YA MCHEZO-Fid Q

Na Yohana Blacklista
Fid Q anaendelea kuimenya siri ya mchezo kama kitunguu, bila kuchokoza ile mihemko ya Darwin’s Nightamre. Lakini je, kama kweli siri hiyo ni mfano wa kitunguu, machozi ya Fid yameonekana, au yeye ni mwanaharakati anayevaa suti vitani? Lakini labda harakati hizo anazidi kuziendeleza kwa kutupa mashairi yenye vidokezo vinavyoweza kutusaidia kufumbua siri zilizofichwa.
gesi1
Tukianza na “BIASHARA na SIASA” ni vitu viwili ambavyo vinatakiwa kuwa kama maji na mafuta, lakini rushwa imeviwezesha vitu hivi kuweza kuchanganyika kama maji na sumu. Katika muziki inauma msanii “unapozimwa, ili ufunikwe na asiyeweza”, hivyo hivyo kwenye siasa, “ukiwa unang’ara ujue kuna kinara”. Rushwa imesaidia wenye fedha kuhonga na kuweka watu wao (wasanii na viongozi), hata kama hawana vigezo. Hili linafanana na kuuwawa kwa Sankara wa Burkina Faso na hata Lumumba kule Kongo na serikali za magharibi, na kisha kumuweka Mobutu Sese Seko madarakani kulinda na kuziendeleza sera za mabepari.
Vinara wa kwenye muziki hawapo tofauti sana. Wao wanahakikisha wasanii wanabaki na “donge la njaa”, ili kuweza kuendelea kuwanyonya kirahisi. Wizi wa “power window” na “rimz za dimpoz” ni kielelezo tosha cha “njaa” waliyonayo wasanii. Pia inawezekana tamaa na kutaka kuwa kama wasanii wa Marekani (utandawazi) ndicho kinachowasukuma. Rimz ni anasa, hasa ukizingatia hazileti “bingo, mshiko”.
Fid amejenga hoja ya msingi hapo, kuwa rimz ni anasa, pia ni udhibitisho wa njaa waliyonayo wasanii. Lakini tusisahau, mabadiliko hayaletwi na matumbo yaliyovimbiwa kwa shibe, bali yanayoganga njaa. Sidhani kama vinara watajisalimisha, bila wenye njaa kuamua matumbo yameunguruma vyakutosha.
“KIDUMU CHAMA CHA MASELA”. Mapinduzi ya dhati yalishapita na huu uhuru ni uhuru wa kutilia mashaka, kwani umetupa tu bendera, kama anavyodai Fid. Kuna ukweli, kutokana na imani kuwa nchi za Magharibi bado wanatawala nchi za Afrika kupitia ufadhili na uwekezaji. Hapa tena, Fid anajenga hoja ya msingi, lakini hachanganui ni vipi nchi za Afrika zitaendelea bila uwekezaji? Pili, katika huu ukoloni mambo leo, nani wa kulaumiwa, sisi au wawekezaji, manake hawajikaribishi wenyewe.
fid&kikwete1
“Kidumu chama cha MASELA”, “tuone kufuru za wenye hela”. Hapa sasa siri ina utata kidogo. Kama hawa masela ndio wale wazee wa enzi zile za mapinduzi ambao leo hii ni wachakachuzi, hivyo je, ni sahihi tutulie tu na kuwatizama wakifanya kufuru? Wajenzi hawa wa matabaka si wao pia ni wakoloni wa kileo? Kampeni zao wanafanya kufuru ya fedha ili kuendelea kushika nyadhifa zao. Fedha zao kweli zina kufuru, kwani si zinawakodisha mpaka wanaharakati? Hili sio geni, kwani hata wasomi wetu hutumiwa na wawekezaji kuwasaidia katika unyonyaji wao. Kuna tofauti gani na wasanii wa nje ambao huthaminiwa kwa kulipwa maradufu zaidi ya wasanii wa hapa nyumbani?
“Tanzania ni demu wa mtungo”, kutokana na wawekezaji kuja kutoka kila kona, na kuchota rasilimali zetu bila sisi kufaidika, “MAENDELEO ni ile ndoto…MWEKEZAJI ashaipuuza..”. Lakini sisi wenyewe hatuli nchi yetu mtungo? Kwa mfano, mafisadi mpaka wasomi wanaotumikia mabepari n.k. Ukisoma kitabu cha Africa Unchained cha George Ayittey wa Ghana, utaona ni jinsi gani sisi wenywe ni tatizo hasa kizazi cha Hippos. Fid analigusia hili kama ifuatavyo.
Viongozi na wananchi tumekuwa kama walevi, “tungi saa zote”, tena kwa makusudi. Huu mstari unajenga picha ambayo inachekesha kidogo, lakini ni mkali. “Hangover” kawaida humfanya mtu kujisikia kuumwa. Hivyo ili kuepuka kujisikia kuumwa huko, lazima mlevi aendelee kuwa tungi. Tunaendelea kujidanganya kuwa mambo yanaenda vizuri nchini, wakati hali halisi inakinzana na hilo. Sidhani kama viongozi hawaifahamu hali halisi, bali wanafanya makusudi kutokana na maslahi yao. Msikilize Mh. Nape kwa makini, hasa anapogusia kwenye suala la umeme (19:00).
Wananchi kwa upande mwingine inawezekana ni kweli wanakuwa walevi kukimbia misongo ya maisha, japo kwa muda mfupi. Misongo hiyo sidhani kama ni illusion. Ubepari “unafanya vijana wanaumia”. Nakubaliana kidogo na Fid kuwa tunalewa ili tuepuke kufanya maamuzi magumu, kama kutoka nje ya gari na kulisukuma. Lakini kwanini tusukume gari bovu? Mwandishi Ngugi wa Devil On The Cross, na yeye kwenye riwaya yake hiyo anatumia istiari yamatatu mkweche aina ya Ford aliloachiwa Mwauru. Matatu hii inajaza abiria kupindukia. Ngugi anaifananisha matatu hii na walichoachiwa viongozi wengi wa Afrika na wakoloni walipoondoka na labda uendeshwaji wa Matatu hii ina akisi jinsi serikali nyingi za Afrika zinavyo ongozwa. Matatu kama hii si hatari kwa usalama wa abiria wake?
Tukibaki kwenye dhana ya uongozi, Fid anasema kutafuta ukweli, au hata kujaribu kuleta mabadiliko inaweza ikawa “ni sawa na kumenya kitunguu”. Kitabu cha Marehemu Chinua Achebe kinachoitwa No Longer At Ease kina mfano mzuri wa hili. Muhusika Obi katika riwaya hiyo anajaribu kupinga rushwa, lakini maisha yake yanakuwa magumu mpaka anajikuta na yeye anapokea rushwa, kwani rushwa imekidhiri mpaka imekuwa sehemu ya maisha ya jamii yake.
Hili tunaliona pia kwenye riwaya ya Ayi Kwei Armah inayoitwa The Beautiful Ones Are Not Yet Born. Ayi Kwei anatoa mfano wa mapipa ya takataka ambayo yanafurika takataka, mpaka yenyewe yanakuwa chanzo cha kuchafua jiji, badala ya kuliweka safi. Fid hapo anakuambia, “daily tunafeli na POLITICAL institutions”, ambazo ndiyo hayo mapipa ya taka. Sasa jaribu kupeleleza kwanini mapipa ya taka nayo yamegeuka kuwa takataka uone upelelezi wako utafika mbali kiasi gani. Kwa upande mwingine, kuna waandishi wa habari ambao nao ni wamenya vitunguu, kwa habari zao za kutafuta ukweli, kwa kufichua maovu. Wengi hujikuta matatani na hata kupoteza maisha wakijaribu kufanya kazi yao. Kwa bahati mbaya au nzuri, hakuna harakati zisizokosa misukosuko.
Kitunguu (ubepari na utandawazi) ni muhimu kimenywe au tutabaki kuwa watumwa tunaojiona tuko free. Lakini pia, wengi kama Fid hawagusii mazuri ambayo yametokana na utandawazi pamoja na ubepari. Lakini je, tatizo pekee ni ubepari na utandawazi, au tatizo zaidi lipo kwenye uongozi mbovu ambao unashindwa kudhibiti mabaya ya ubepari na utandawazi?.
NYERERE
Tukirudi nyuma katika kipindi cha ujamaa, watu walikuwa wakimuita Nyerere Mussa. Fid anasema “walijivisha U-MUSSA..fimbo zao hazikugeuka nyoka”. Nyerere alifanikiwa kuipatia Tanzania uhuru, lakini wengi wanahoji kuwa sera yake ya ujamaa ilirudisha Tanzania nyuma kimaendeleo na kiuchumi. Mawazo ya Ayyitey na Fid na hata ya riwaya nyingi zilizo andikwa baada ya uhuru, zinaakisi mtazamo huo juu ya baadhi ya serikali za Afrika baada ya ukoloni. Wengi waliona, pamoja na viongozi wa kipindi hicho kuweza kupigania uhuru, lakini walishindwa kuleta maendeleo katika nchi zao (kuzifikisha kwenye nchi ya ahadi kama Mussa kwa Waisraeli).

Hoja zao ni hoja za upande mmoja. Leo hii, ambapo tuna rasiliamali ya wasomi na miundombinu, ni mabadiliko makubwa kiasi gani yaliyoletwa hasa katika kupunguza umasikini? Pia tujiulize, wale Mussa wa kipindi kile na hawa Miungu watu wa leo bora nani? Miungu watu wanaamua “nani leo atatoka”, wakati ukimsikiliza Nyerere, utagundua alikuwa mwana demokrasia aliyepigania miko na maadili ya uongozi. Radio kubwa na watangazaji wanaamua msanii gani asikike na yupi asisikike. Wao ndio waamuzi, huku maamuzi yao yakisukumwa na hongo badala ya vipaji. Tujiulize pia, je, watangazaji wa radio kuwa mameneja wa wasanii nalo linachangia katika tatizo?
Mwisho ni muhimu kurejea kwenye swali analoliuliza Fid Q, “je hizi track za harakati ni ujinga?”. Swali hili la Fid linanikumbusha mstari wa Lupe Fiasco akisema “I know you’re sayin Lupe rappin about the same shit, well, that’s cause aint shit changed bitch”. Fid ni kama anajitilia shaka, labda juhudi zake hazina manufaa. Ni muhimu tumsikilize Fid na tumuulize maswali. Kwa mfano, “kuna uhuru wa ukweli (Afrika) msidanganyee na illusion”. Uhuru wa ukweli ni upi, nchi gani wenye nao, au Fid anazungumzia utopia? Mfano mwingine Fid anasema “siri ya mchezo naijui mimi..tu na hakuna mwingine”. Hii ni kweli? Mh.Sugu na Anaconda Lady Jaydee je, au harakati zao ni tofauti na za Fid?

0 maoni:

Post a Comment