ALIYEWAHI kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha (45) amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akikabiliwa na mashitaka ya kutumia lugha ya matusi kwa maofisa wa Jeshi la Polisi.
Masha alifikishwa mahakamani hapo jana saa 4:37asubuhi akiwa amevaa fulana nyeusi na suruali ya rangi ya bluu na kuhifadhiwa mahabusu hadi saa 9:00 mchana alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka mbele ya Hakimu Mkazi, Waliarwande Lema.
Baada ya kusomewa mashitaka alipelekwa mahabusu katika gereza la Segerea baada ya upande wa Jamhuri kuomba kwenda kuhakiki nyaraka za wadhamani wake kama ni halali.
Awali, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon, alidai kuwa Agosti 24, mwaka huu katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, Masha ambaye ni Wakili wa Kujitegemea, alitoa lugha ya matusi kwa maofisa wa Jeshi la Polisi.
Alidai kuwa Masha alitoa lugha ya matusi kwa Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Juma Mashaka na wenzake akiwaambia ni “wajinga, washenzi waonevu, hamna shukrani, huruma wala dini,” maneno ambayo yangesababisha uvunjifu wa amani.
Masha alikana mashitaka na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika. Hakimu Lema alisema mshitakiwa atapata dhamana endapo atakuwa na wadhamini wawili wa kuaminika na kila mmoja atasaini hati ya Sh milioni moja.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliomba Mahakama ikazihakiki nyaraka za wadhamini zilizowasilishwa na wadhamini wa Masha ili kujiridhisha kama ni halali. Mahakama ilikubali ombi hilo na Masha alipandishwa kwenye gari la Magereza na kupelekwa mahabusu katika gereza la Segerea.
Masha alichanganywa na washitakiwa wengine na kuondoka katika eneo hilo wakiwa chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi waliovaa kiraia na wengine wenye sare wakiwa na silaha.
0 maoni:
Post a Comment