CHAMA cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na ushauri (TUICO) kimekiri kuwepo kwa migogoro mingi baina ya wafanyakazi na waajiri wao. Hayo yalisemwa jana na wakili wa chama hicho kutoka makao makuu Dar es Salaam, Noel Nchimbi, kwenye mkutano mkuu wa TUICO kwa mkoa wa Shinyanga.
Mkutano huo ulikwenda sanjari na uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa kuwakilisha ngazi ya kanda na taifa. Nchimbi aliwatoa hofu wafanyakazi hao kuwa licha ya migogoro kuwa mingi kutokana na chama kuwa na wanachama wengi, wameweza kukabili kesi zilizopo na kutekeleza matakwa ya wanachama wao.
“Leo katika mkutano huu tutawapata viongozi wapya ambao ni wawakilishi wa wafanyakazi. Kinachotakiwa ni mahusiano mazuri na serikali, hata pale migogoro inapotokea mnamalizana kiheshima. Bado kuna kero ya makato ya kodi kwa wafanyakazi na haya kuyamaliza ni sisi wenyewe kuyasemea.Tumekuwa tukisema tunaowachagua kwenda bungeni kutuwakilisha wanajisahau,” alisema Nchimbi. Katibu wa chama hicho mkoa wa Shinyanga, Fabian Samkumbi, alisema chama kwa mkoa huu kina wachama zaidi ya 445 ila kuna changamoto ya baadhi ya wafanyakazi kutaka kujitoa na wengine kuwa wagumu kujiunga.
Hata hivyo, alisema uelimishaji unaendelea. Wajumbe waliohudhuria kwenye uchaguzi huo walikuwa 33 ambapo kwa nafasi ya uenyekiti mkoa, Fue Mrindoko alitetea nafasi yake tena kwa kuibuka mshindi huku akiwa hana mpinzani kwenye nafasi hiyo.
Walioshinda kuwakilisha mkutano mkuu taifa na sekta zao kwenye mabano ni Songoro Yusuph (viwanda), Gaston Itumba (biashara), Yusuph Bula (fedha) na Moses Dagobert (huduma na ushauri). Kadhalika kuna waliochaguliwa kwenye mkutano wa Kanda ya Ziwa katika sekta hizo.
0 maoni:
Post a Comment