Ofisa Mwandamizi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), George Kashura (kushoto) akimkabidhi Katibu Mkuu wa chama cha ACT- Wazalendo, Samson Mwigamba fomu za uteuzi wa mgombea urais na makamu wa rais kwa niaba ya wagombea wa nafasi hizo kupitia chama hicho, Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis
Sintofahamu imetanda ndani ya Chama cha ACT – Wazalendo juu ya hatima ya mgombea wa urais baada ya mgombea aliyependekezwa na kuchukuliwa fomu ya kuomba uteuzi, Profesa Kitila Mkumbo kuikataa nafasi hiyo.
Mapema jana saa 4.30 asubuhi, Katibu Mkuu wa chama hicho, Samson Mwigamba alitinga katika Ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuchukua fomu bila ya kuwa na Profesa Kitila na kueleza kuwa mgombea wao huyo yupo safarini.
Mwigamba alisema alikwenda kuchukua fomu hiyo kwa niaba ya chama na bila kusindikizwa na viongozi wengine kwa kuwa walikuwa kwenye vikao vya ndani vilivyokuwa vikiendelea.
Muda mfupi baada ya Mwigamba kuchukua fomu hizo, Profesa Mkumbo aliandika katika ukurasa wake wa Facebook kuwa anawashukuru makada na Kamati Kuu ya chama hicho kumwamini na kumtaka agombee urais lakini kwa sasa hayupo tayari.
Katika ujumbe huo ambao baadaye alikiri kuuandika, Profesa Mkumbo alisema Kamati Kuu ilituma ujumbe maalumu nyumbani kwake juzi kuzungumza na familia na jamaa zake juu ya ombi hilo na kubainisha kuwa amekuwa akitafakari uwezekano wa kugombea nafasi hiyo baada ya juhudi za kutafuta mgombea kushindikana.
“Nimefanya mawasiliano mapana katika familia, ndani ya chama, chuoni ninapofanyia kazi, kanisani kwangu na kwa watu na taasisi mbalimbali ninazohusiana nazo.
“Baada ya tafakari na mawasiliano mapana, nasikitika kusema kwamba sina utayari na maandalizi ya maana ya kisaikolojia, kifamilia na kisiasa kuniwezesha kugombea nafasi ya urais katika uchaguzi huu,” alisema Profesa Mkumbo.
Alisema anajua bayana amewaangusha lakini anaamini kwamba wafuasi hao wataheshimu uamuzi wake, hivyo hawataacha kuthamini mchango alioutoa katika chama hicho kwa sababu amekataa kugombea urais.
Alishauri chama kiwaombe wanachama wengine waandamizi kuchukua jukumu hilo, akiwamo Mwenyekiti, Anna Mghwira, huku akiwataka makada wa ACT –Wazalendo kutomtuhumu kwa lolote juu ya uamuzi wake.
Kukataa kwa Profesa Mkumbo kunakipa kazi chama hicho kutafuta mbadala wa mgombea huyo ambaye ni moja ya waasisi wa chama hicho chenye makao yake makuu, Kijitonyama jijini hapa.
Hata hivyo, Mwigamba alipoulizwa mbadala baada ya mgombea waliyemchukulia fomu kukataa, alisema hawadhani kuwa Profesa Mkumbo atakataa na ikitokea hivyo watamtafuta kada mwingine agombee.
Mwigamba alisema mgombea mwenza aliyetarajiwa ni kada wa muda mrefu wa ACT – Wazalendo aitwaye Hawra Shamte.
''Alipotakiwa kueleza kwa kina iwapo jina la mgombea mwenza huyo ni linahusiana na Mhariri wa gazeti la Mwananchi, Hawra Shamte, Mwigamba alisema: “Siyo huyo na kiufupi yeye (mgombe mwenza) na mgombea urais tutawatangaza baada ya kikao cha dharura cha Kamati ya Uongozi kukamilika leo (jana) au kesho (leo).”
Shamte alipoulizwa kuhusu mpango huo, alisema hajui jambo hilo na kwamba jina hilo huenda halihusiani naye kwa kuwa yeye si mwanachama wa chama chochote.
Makada wavamia ACT
Baada ya taarifa ya Profesa Mkumbo kukataa kuzagaa, makada zaidi ya 200 wa ACT – Wazalendo walitinga katika ofisi cha chama hicho wakiwa katika maandamano wakishinikiza agombee.Maandamano hayo yalianzia jirani na Ofisi ya Tume ya Sayansi na Teknolojia Kijitonyama, wilayani Kinondoni hadi katika ofisi za chama hicho zilizopo umbali wa kilomita moja.
Waandamanaji hao wakiwa na bendera za chama hicho walifika katika ofisi za chama hicho saa 6.10 mchana na kutishia kuvunja mlango wa ofisi lakini walizuiwa na wenzao waliokuwa ofisini.
Baada ya azma hiyo kushindwa, waliendelea kuimba nyimbo mbalimbali za kumshinikiza Profesa Mkumbo kuwania urais huku wakiwa na mabango yenye ujumbe wa aina mbalimbali ukiwamo “…Bora ofisi ifungwe kama hatuwezi kusimamisha mgombea urais.”
Wengi wa waandamanaji hao ambao ni vijana kati ya miaka 20 na 30 waliendelea kuimba: “Zitto na Kitila turudishieni chama chetu kama mmeshindwa kuweka mgombea urais. Kitila Mkumbo tumia busara na hekima wewe ni rais 2015.”
Katika hali ya kushangaza, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Shaaban Mambo aliingia katika ofisi hizo saa 6.30 mchana na kupokewa kwa shangwe na vijana ambao waliimba huku wakisema, “karibu Profesa Kitila, Kitila, Kitila.”
Baada ya Mambo kuingia ndani, ndipo baadhi ya vijana wakaanza kuwaeleza wenzao kuwa yule hakuwa Profesa Kitila.
Baadaye ofisi za chama hicho ziligeuka ‘uwanja wa vita’ kwa vijana hao baada ya kuanza kugombania maji na biskuti zilizokuwa zikitolewa katika ofisi hiyo.
Mmoja wa wafuasi wa chama hicho aliyekuwa akigawa vinywaji hivyo alishindwa kuhimili vurugu za vijana hao na kuamua kuwarushia juu chupa za maji na biskuti.
Na Nuzulack Dausen na Raymond Kaminyoge
0 maoni:
Post a Comment