"Ni Mungu tu Pekee Ndiye Awezayekuniokoa...!!!",INASIKITISHA SANA ,HUJAFA HUJAUMBIKA


NI kweli hujafa hujaumbika! Leo unaweza kuamka mzima lakini kesho ukafika ukiwa huwezi! Unaweza kusema ‘mi naumwa’ kumbe hujawaona wagonjwa wenyewe. Ukishawaona, utagundua kuwa, ugonjwa wako hahuitaji tabibu.


Kijana Abel Revocatus Machanga (23), anayeishi na wazazi wake, Ukonga ya Mombasa jijini Dar, anaugulia mateso makali kufuatia kupata ugonjwa wa ajabu ulioyafanya macho yake kutoka nje umbali wa pingili ya vidole vya mkononi na kushindwa kupumua sawasawa.

Akizungumza kwa uchungu wa mateso ya mwanaye, baba mzazi wa kijana huyo, mzee Revocatus Machanga alisema kuwa maisha ya nyumbani hapo yamekuwa ya huzuni kwani kila anapomuangalia mtoto wake huyo, machozi yanamtoka.


UGONJWA ULIPOANZA
Mzee Machanga alisema kuwa, mtoto wake huyo alianza kuugua Novemba 2014. Anasema kijana huyo alianza kwa kulalamikia maumivu ya kichwa kwamba kinamgonga sana. Pia macho yalianza kuvimba kidogokidogo, yeye akajua ni ugonjwa wa macho tu na yatapona.

HALI MBAYA, AMPELEKA HOSPITALI
Mzazi huyo aliendelea kusema kuwa, siku zilivyozidi kwenda mbele, ndivyo macho hayo yalivyokuwa yakizidi kuvimba. Ndipo aliamua kumpeleka Hospitali ya Macho ya Comprehensive Community Based Rehabilitation in Tanzania (CCBRT) ambapo waligundua kuwa macho hayana tatizo ila mishipa ya fahamu ndiyo ina kasoro, hivyo walishauri apelekwe Hospitali ya Taifa Muhimbili Taasisi ya Magonjwa ya Mifupa ‘Moi’ (Muhimbili Orthopeadic Institute) ambako kuna wataalam wa mishipa ya fahamu.

MAJIBU YA MOI
“Tulipofika Moi walimwangalia, wakampangia siku ya kumuona ambapo ilikuwa kama mwezi mmoja mbele. Lakini tulipokuwa tukisubiri muda wa kumuona, macho yalizidi kuwa katika hali mbaya ambapo yalitoka nje kabisa.

ATAKIWA KUPASULIWA
(huku akifuta machozi) mzazi huyo aliendelea kusema: “Siku ya kumwona daktari ilifika, tukaenda. Walimpima na kugundua kuwa, ana uvimbe kwenye ubongo wa mbele. Wakasema wanaweza kumfanyia upasuaji lakini masharti waliyotueleza kuhusiana na upasuaji huo ni magumu sana.

“Walisema kuwa akifanyiwa upasuaji huo lazima awekwe chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) kwa muda wa siku kumi na nne na kwamba atatolewa macho yote na sura yake itabadilika kitu ambacho kilinifanya nijishauri tena.”

Mzazi huyo ambaye muda mwingi kwake ni kilio, aliendelea kusema kuwa awali walijua tatizo kubwa ni kansa lakini kumbe haikuwa hivyo na kwa sasa, uvimbe huo umesababisha pua za kijana huyo kuziba na meno kuuma kiasi ambacho anashindwa kula chakula zaidi ya uji na mtori tu.

BABA AULIZIA MATIBABU INDIA
Mzee Machanga alisema kuwa, ilibidi aulizie hospitali za India zinawezaje kufanya upasuaji huo ambapo wenye uzoefu walisema kijana huyo anaweza kufanyiwa upasuaji kwa shilingi milioni 40 kitu ambacho wao kama familia hawawezi kwa kuwa mzazi huyo na yeye ni mgonjwa, hafanyi kazi yoyote.

MGONJWA AZUNGUMZA KWA TABU
Akizungumza kwa tabu sana na gazeti hili, Abel alisema anatamani kuwa mzima kama zamani ili aweze kutimiza ndoto zake kwa kusoma sana. Alikuwa akisomea masoko kwenye Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) cha jijini Dar.

“Hii hali mimi inaniuma sana. Kuna wakati najiuliza sasa kwa nini naishi kama kuishi kwenye ni kuteseka kiasi hiki. Kwa nini mimi? Ingawa najua Mungu ana mipango yake na ananiona ninavyoteseka.

“Ndoto zangu zote zimekatika kabla ya kufika mwisho. Ni kama mtu anayeota ndoto akiwa amelala halafu akaamshwa ghafla. Nilikuwa nikisoma pale CBE ili na mimi niwe na maisha mazuri, niwasaidie wazazi wangu. Kwa sasa ndoto zangu zimeishia hapa. Lakini kwa jinsi baba alivyonihangaikia ili nipone, naamini kwa sasa wa kuniokoa ni Mungu tu,” alisema Abel.

KAMA UMEGUSWA
Ndugu msomaji, kama umeguswa na tatizo la kijana Abel, unaweza kumsaidia. Baba yake ameeleza kila kitu. Kinachotakiwa ni pesa tu. Na Kutoa ni moyo si utajiri. Kama unatoa, unaweza kutumia namba za simu za baba yake ambazo ni; 0713 275740, 0784 275740, 0752 275740. 

0 maoni:

Post a Comment