UPELELEZI wa kesi ya uhujumu uchumi ulioisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 12.7 inayomkabili aliyekuwa Kamishna wa Forodha na Ushuru wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Tiagi Masamaki na wenzake, haujakamilika.
Wakili wa Serikali, Diana Lukondo alidai hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi hiyo ilipotajwa. Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Huruma Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 13 mwakani itakapotajwa tena.
Mbali na Masamaki washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni vigogo wengine wa mamlaka hiyo, Mkuu wa Kituo cha Huduma kwa Wateja TRA, Habibu Mponezya, Meneja Udhibiti wa Forodha na Ufuatiliaji, Burton Mponezya, Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Hamisi Omary (48) na Haroun Mpande wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta TRA.
Wengine ni wafanyakazi wa Bandari Kavu (ICD) ya Azam, Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha ICD Azam, Eliachi Mrema (31), Meneja wa Oparesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Adolf Louis (39) na Meneja wa Azam ICD, Ashraf Khan (59).
Washitakiwa saba wameachiwa kwa dhamana huku Mpande akiendelea kusota rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana. Masamaki, Habib Mponezya na Burton Mponezya wao waliachiwa huru kwa dhamana.
Wanadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Juni Mosi na Novemba 17, mwaka huu sehemu isiyofahamika, walikula njama za kuidanganya Serikali kuhusu Sh bilioni 12.7, kwa madai kuwa makontena 329 yaliyokuwa kwenye ICD ya Azam yametolewa baada ya kodi zote kufanyika, jambo ambalo si kweli.
0 maoni:
Post a Comment