MBWANA SAMATTA AKUTANA NA NAPE NNAUYE NYUMBANI KWAKE


Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania Mbwana Samatta leo amekutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo Mh. Nape Nnauye kwenye ofisi ya Waziri huyo kwa ajili ya kumuaga kwa niaba ya serikali kabla ya kuelekea nchini Nigeria kuhudhuria sherehe za ugawaji wa tuzo za wachezaji bora wa Afrika.

Samatta amesema anatambua umuhimu wa mchango wa serikali katika kuchangia mafanikio yake pamoja na soka la Tanzania kwa ujumla na kuongeza kuwa, endapo atafanikiwa kutwaa tuzo hiyo basi haitakuwa ya kwake binafsi bali ni ya taifa zima.
“Kama nitafanikiwa kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika tuzo hiyo haitakuwa ya kwangu peke yangu bali itakuwa ni ya watanzania wote pamoja na Tanzania kama nchi”, amesema Samatta ambaye yupo kwenye orodha ya wachezaji watu ambao wameingia fainali ya kuwania tuzo ya mchezaji bora Afrika kwa wachezaji wa ligi za Afrika.

“Kabla ya kwenda sehemu yoyote ile ni lazima upate baraka za wazee ndiyomaana nimekuja hapa kuaga na kuchota baraka za serikali kwa niaba ya Wiara inayohusika na michezo kabla ya kuelekea Nigeria kuwania tuzo ya mchezaji bora Afrika”.

Kwa upande wa Mh. Nnauye yeye amesema serikali ipo bega kwa bega na Samatta  pamoja na wanamichezo wote huku akimtakia kila laheri mchezaji huyo katika kinyang’anyiro hicho.

Nnauye pia amesema serikali inapambana ili kuhakikisha wanamichezo wote wanafaidika kutokana na kazi zao na itapambana na wale wote ambao wamekuwa wakila kupitia jasho la wanamichezo.

“Kwa niaba ya serikali, nakupongeza kwa hatua uliyofikia kwani hadi hapo umelitangaza vyema taifa letu lakini pia hata tuzo ambayo unawania endapo utaitwaa itazidi kukutangaza wewe lakini pia nchi yetu itatangazwa kupitia wewe”, amesema Mh. Nauye.

“Lakini serikali sasa inasimamia vyema maslahi ya wanamichezo wote ili wafaidike na kile ambacho wanakitolea jasho na tunataka kupambana na wale wote ambao wanajinufaisha kupitia jasho la wanamichezo”.

Samatta pia amempongeza Mh. Nape Nnauye kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge pamoja na kuteuliwa kuwa waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo.



Tuzo za wachezaji bora Afrika zitatolewa nchini Nigeria January 7, 2016 ambapo Samatta anawania tuzo hiyo ya mcheaji bora Afrika kwa wachezaji wa ligi za Afrika akiwa pamoja na Bahgdad Bounejah (Etoile du Sahel, Tunisia) Algeria na Robert Kidiaba (TP Mazembe, Congo DR) Jina la Samatta limeingia kwenye orodha ya wachezaji watatu wanaowania tuzo hiyo baada ya kuisaidia timu yake ya TP Mazembe kutwaa kombe la klabu bingwa Afrika huku yeye akiibuka mfungaji bora wa michuano hiyo.

0 maoni:

Post a Comment