Polisi mkoani Morogoro imefanikiwa kumtia mbaroni Nehemia Nashoni kwa tuhuma ya kukutwa akiwa na pembe za ndovu vipande vitano yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 100 kwenye nyumba ya kulala wageni ya B-Z iliyopo Nane Nane, Manispaa ya Morogoro.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea Novemba 8, mwaka huu saa nne usiku maeneo ya Nane Nane katika Hoteli ya B-Z iliyopo Manispaa ya Morogoro.
Alisema kuwa, askari Polisi wakiwa doria walipokea taarifa za kuwepo kwa mtu mmoja aitwaye Nehemia Nashoni akiwa na pembe za ndovu na kufanikiwa kumkamata. Kamanda huyo wa Polisi wa Mkoa alisema, baada ya kumpekua alikutwa akiwa na pembe za ndovu vipande vitano vyenye uzito wa kilo 20 katika chumba namba 104 alichokuwa amekodi katika hoteli hiyo.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo thamani za pembe hizo ni zaidi ya Sh milioni 100. Kamanda Matei alisema kuwa hatua zinazofuata ni za kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo na alitoa wito kwa wananchi wa Morogoro kuendelea kushirikiana na Polisi katika kuwafichua wahalifu na uhalifu.
0 maoni:
Post a Comment