Polisi mjini hapa wameyasambaratisha maandamano ya watu wasiofahamika waliokuwa na mabango ya kutaka muda wa uandikishwaji wa wapigakura kuongezwa.
Watu hao, ambao polisi iliwaita ‘wahuni’, waliandamana saa tatu asubuhi kwenye Barabara ya Sokoine.
Haikuweza kufahamika mara moja watu hao walitoka wapi, kwani wenyeviti wa mitaa ya kata zote hawakuweza kuwatambua.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema walilazimika kutumia nguvu kuvunja maandamano hayo kwa vile hayakuwa halali.
Sabas alisema watu hao ni kundi la wahuni lililozuka kutaka kusitishwa uandikishaji wa wapigakura.
Diwani wa Kata ya Sombetini, Ally Bananga alisema hakuwa na taarifa na maandamano hayo, lakini hashangai kutokea kwake.
“Sitashangaa watu kuandamana, kwani wamechoshwa na tabia ya watendaji kuwarudisha nyumbani. Watu wanafika asubuhi kituoni wanaambiwa warudi nyumbani kwa sababu hawakuandikisha majina yao,” alisema Bananga.
Mwenyekiti wa Mtaa wa JR, Jackson Mollel aliitaka tume kutoa mwongozo wa kuwasaidia wananchi kujiandikisha sehemu husika.
0 maoni:
Post a Comment