Na Yohana
MGOMBEA mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Hassan Suluhu, amemnadi mgombea urais wa chama hicho, Dk John Magufuli kwamba hana mchezo na vitendo vya rushwa jambo litakaloleta maendeleo zaidi.
Samia ambaye alitoa ahadi mbalimbali, alisema hayo jana katika mkutano wa wa kampeni uliofanyika Marangu Mtoni, katika Jimbo la Vunjo, wilaya ya Moshi. Alisema kwa kuwa mgombea urais wa chama hicho, Dk Magufuli, hana mchezo na vitendo vya rushwa, maendeleo zaidi yatazidi kuonekana wilayani Rombo na taifa kwa ujumla.
Alisema CCM imefanyakazi kubwa katika maendeleo huku akitolea mfano mitandao ya barabara ambayo imeunganisha mikoa na hivyo kurahisisha sekta ya uchukuzi na usafirishaji wa bidhaa kwa wafanyabiashara.
Alisema Ilani ya chama hicho imefafanua namna itakavyotekeleza miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kukabiliana na changamoto zinazokabili jamii . Mgombea huyo baada ya kusikiliza kero zinazowakabili vijana, wanawake na jamii hiyo kwa ujumla kutoka kwa mgombea ubunge wa chama hicho Innocent Shirima, aliahidi kutoa pikipiki 30 kwa ajili ya kuinua vijana katika eneo la Marangu Magharibi, jimboni Vunjo, mkoani Kilimanjaro.
Aidha mgombea huyo amewaahidi wakazi wa Vunjo kuwa binafsi atasaidia kutatua tatizo la bei ndogo ya kahawa linalowakabili wakulima wa eneo hilo, ikilinganishwa na wakulima wa zao hilo, nchini Kenya.
Hali kadhalika, aliahidi kukamilisha ujenzi wa soko la Himo, kuwawezesha wafanyabiashara wa eneo hilo, kufanya biashara na jirani zao wa Kenya pamoja na Sudan Kusini. Akiwa katika mkutano wa hadhara Rombo, Samia aliwataka wakazi wa eneo hilo kuipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25.
0 maoni:
Post a Comment