Na Yohana
WATU nane wamethibitishwa kufariki kwa ugonjwa wa kipindupindu na wengine 262 wameambukizwa maradhi hayo katika mkoa wa Dar es Salaam na Morogoro.
Waziri wa Afya na Usatwi wa Jamii, Dk Seif Rashid akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwenendo wa maradhi ya ugonjwa huo uliozuka hivi karibuni alisema hadi kufikia jana, kwa mkoa wa Dar es Salaam, watu saba wamefariki na wengine wapatao 230 tayari wameambukizwa ugonjwa huo.
Waziri wa Afya na Usatwi wa Jamii, Dk Seif Rashid “Tangu ugonjwa huu uanze Agosti 15 mwaka huu, idadi ya wagonjwa walioripotiwa kwa mkoa wa Dar es Salaam ni 230 na vifo vya watu saba,” alisema Dk Rashid. Kwa mujibu wa Dk Rashid, maeneo yalioathirika zaidi na ugonjwa huu kwa mkoa wa Dar es salaam ni pamoja na maeneo ya Makumbusho, Kimara, Tandale, Manzese, Saranga na Magomeni.
Maeneo mengine ni Mwananyamala, Kibamba, Kigogo, Goba, Mburahati, Kinondoni na Kijitonyama kwa manispaa ya Kinondoni. Kwa upande wa manispaa ya Ilala, maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Buguruni, Majohe, Chanika, Sharifu Shamba na Tabata, wakati katika manispaa ya Temeke, maeneo yalioathirika ni Mtoni kwa Azizi Ally, Keko na Yombo Vituka.
Katika mkoa wa Morogoro, Dk Rashid alisema ugonjwa huo ulianza mkoani hapo Agosti 17 mwaka huu na hadi kufikia Agosti 24, mtu mmoja amefariki dunia na wengine 32 wameambukizwa.
0 maoni:
Post a Comment