CHAMA CHA ACT WAZALENDO KUZINDUA KAMPENI JUMAPILI...!!

CHAMA cha ACT-Wazalendo kinatarajia kuzindua kampeni zake Jumapili Agosti 30, katika viwanja vya Mbagala Zakhem, jijini Dar es Salaam.

 Ofisa Habari wa chama hicho, Abdallah Khamisi alimwambia mwandishi wa habari hizi kwa njia ya simu kuwa mgombea urais, Anna Mghwira na mgombea mwenza wake, Hamad Mussa Yusuf watamwaga sera zao kwa wakazi wa Dar es Salaam siku hiyo.

Alisema baada ya kuzindua kampeni hizo katika mkoa wa Dar es Salaam wataelekea katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Iringa na kumalizia mkoa wa Katavi Septemba 3. Khamisi alisema Septemba 5 na 6 watakuwa Kigoma mjini, Septemba 7 Tabora mjini na Septemba 8, Shinyanga.
"Tutaendelea na ratiba yetu katika mikoa mingine hadi tutakapohitimisha kampeni zetu," alisema. Wakati huo huo, Ratiba nyingine iliyotolewa na vyama vilivyo katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) inaonesha kwamba watazindua rasmi kampeni zao Agosti 29 katika viwanja vya Jangwani jijini Dar es Salaam, ambapo Chama Cha Mapinduzi (CCM), mwishoni mwa wiki walizindua kampeni zao.


Wagombea waliosimamishwa na umoja huo ni Edward Lowassa ambaye ni mgombea urais na Juma Duni Haji, mgombea mwenza, wote kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

0 maoni:

Post a Comment