Vyombo vya habari vya Ubelgiji vinaituhumu serikali ya Rwanda kuwa inatekeleza njama za kuua wapinzani wake walio nchini Ubelgiji.
Aidha radio ya Kimataifa ya Ufaransa RFI siku ya Jumamosi katika tovuti yake ya intaneti iliripoti kuwa kuna makundi ya wauaji walio nchini Ubelgiji.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa makundi hayo ya wauaji yanalenga kuwamaliza wapinzani wa serikali ya Rwanda walio katika nchi za kigeni. Serikali ya Rwanda imetuhumiwa mara kadhaa kuwa imekuwa ikipanga njama za kuwaua wapinzani wake lakini wakuu wa Kigali daima wamekanusha tuhuma hizo.
Faustin Twagiramungu waziri mkuu wa zamani wa Rwandaambaye yuko uhamishoni nchini Ubelgiji hivi karibuni alisema nyumba yake mjini Brussels iliwekwa chini ya ulinzi mkali wa vikosi vya usalama vya nchi hiyo. Aliongeza kuwa ulinzi huo mkali uliendelea kwa muda wa siku tatu na baada ya hapo oparesheni hiyo ikasitishwa pasina kuwepo maelezo.
Naye Judi Rever mwandishi habari Mkanada ambaye huchunguza jinai zinazohusishwa na serikali ya Rwanda amesema kuwahivi karibuni aliwasili Ubelgiji ambapo maafisa usalama nchini humo walipendekeza kuwa wampe ulinzi kwa muda wa masaa 24. Afisa aliyekuwa akiongoza walinzi wake alimdokezea kuwa Ubalozi wa Rwanda mjini Brussels Ubelgiji ni tishio kwa maisha yake.
Serikali ya Rwanda inatuhumiwa kuwa inalenga kuwaua wapinzani wake katika hali ambayo hivi sasa Rais Paul Kagame wa nchi hiyo yuko katika mkakati wa kuhakikisha kuwa anaendelea kubakia madarakani hata baada ya kumalizika muhula wake wa pili mwaka 2017.
Katika uchaguzi wa mwaka 2010 nchini Rwanda, Kagame alishiriki na kupata ushindi kwa duru ya pili baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994. Alichaguliwa moja kwa moja kupitia kura za wananchi kwa mara ya kwanza mwaka 2003. Kwa mujibu wa katiba ya sasa ya Rwanda hawezi kugombea tena urais kwani muhula wake wa sasa unamalizika. Kipengee 101 cha katiba ya Rwanda kimebainisha wazi kuwa rais atahudumu kwa mihula miwili ya miaka saba kila mmoja. Pamoja na hayo Kagame anatekeleza mkakati maalumu wa kubadilisha kipengee hicho ili ashiriki katika uchaguzi wa mwaka 2017. Hivi karibuni wabunge wa Rwanda walianzisha mchakato wa kubadilisha katiba ya nchi hiyo ili Kagame aweze kugombea urais kwa muhula wa tatu mfululizo.
Wakosoaji wa Kagame wanamtuhumu kuwa anadhoofisha demokrasia sambamba na kuwakandamiza wapinzani. Lakini Kagame anapinga tuhuma hizo huku wafuasi wake sugu wakidai kuwa mabadiliko kwa maslahi ya kubakia madarakani Kagame ni takwa la wananchi waliowengi.
Uamuzi wa Kagame kubakia madarakani ni jambo ambalo limekumbana na upinzani mkubwa wa wapinzani. Aidha wanaopinga pendekeozo hilo nje ya nchi hasa Ubelgiji wanahofia maisha yao. Baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, baadhi ya wakuu wa Rwanda walikimbilia uhamishoni katika nchi kama vile Ufaransa, Uingereza na Ubelgiji.Imearifiwa kuwa wapinzani walio nje ya Rwanda wameanzaisha kampeni kubwa dhidi ya Kagame. Hivi sasa rais wa Rwanda anatuhumiwa kuwa anatumia mbinu chafu kuwamaliza wapinzani wake walio ndani na nje ya nchi.
Kwa sasa Rwanda inashuhudia amani na utulivu lakini hitilafu za kikabila baina ya Wahutu na Watutsi zingalipo. Rais Paul Kagame wa kabila la Tutsi hadi sasa amejitahidi kumaliza ua kupunguza hitilafu za kikabila na kwa msaada wa nchi za Magharibi ameweza kuboresha hali ya uchumi wa nchi. Lakini tetesi kuwa anataka kugombea urais kwa muhula wa tatu sambamba na kukuwakandamiza wanaopinga utawala wake wa kiimla ni jambo ambalo linaiweka nchi hiyo katika mkondo hatari.
0 maoni:
Post a Comment