Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
akiwakaribisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo aliyeambatana na
Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe kabla ya kuanza kwa kikao
chao cha pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa
katika kikao cha pamoja na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Naibu
Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo pamoja na Katibu Mkuu wa TAMISEMI
Mussa Iyombe.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiagana na
Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan mara baada ya kumaliza kikao chao
kilicho wahusisha Naibu Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo pamoja na
Katibu Mkuu wa TAMISEMI Mussa Iyombe Ikulu jijini Dar es Salaam. PICHA
NA IKULU
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza
Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa
wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga katika Jiji la
Mwanza mpaka hapo mamlaka husika itakapokamilisha maandalizi ya maeneo
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
Rais
Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo
hilo leo tarehe 06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam huku akionya
kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo aachie
ngazi.
"Kumeibuka
tabia ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwafukuza
Wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine
wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya biashara,
hili jambo sio sawa hata kidogo.
"Sipendi
Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara lakini hakuna
sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au Mmachinga
hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye utaratibu wa
namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza madaraja
ya Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa
kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa
katikati ya mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya
Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita
kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini
na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na
nataka kulirudia kwa mara ya mwisho" amesema Rais Magufuli.
Dkt.
Magufuli ameelekeza kuwa Wamachinga waliondolewa katika maeneo yao
Jijini Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo Halmashauri
ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali
watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha Wamachinga wenyewe.
"Narudia
na hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata Wamachinga wa Mwanza warudi
kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri, Kigamboni
hapa palikuwa na wamachinga eneo fulani wamehama vizuri kweli,
wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya
kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa Wamachinga, lakini Mwanza
imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi
sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa" amesisitiza
Rais Magufuli alipokuwa akiwaekeleza Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe.
Suleiman Jafo na Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe.
Wakati huo huo, Rais
Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara moja zoezi
la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo
katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga na badala yake wachimbaji hao
waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo
hilo ni lake aondolewe.
"Wale
waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo
mwekezaji ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa
Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale wanapata
riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu."Na hizi ndio
ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja
unakwenda kuwafukuza watu 5,000? haiwezekani na wala haingii akilini" amesisitiza Rais Magufuli.
Rais
Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo ambayo
wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo kwa
kutengeneza nyaraka zinaonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla
ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.
Hata
hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa Wamachinga
na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria bali
wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
06 Desemba, 2016
0 maoni:
Post a Comment