NA YOHANA EMMANUEL
Tarehe 9 Disemba Tanzania itaadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania
Bara kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, ambapo Rais wa Jamhuri
ya Muuungano wa Tanzania, Dkt John Magufuli atakuwa mgeni rasmi siku
hiyo.
Ni kwa mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi katika
shughuli ya maadhimisho ya sherehe za Uhuru, zinazofanyika kila mwaka wa
tarehe hiyo kwa kuwa mwaka jana aliahirisha sherehe hizo na kuagiza
kiasi cha fedha walichotakiwa kukitumia siku hiyo aliagiza fedha hizo
zitumike kupanua Barabara ya Morocco – Mwenge jijini Dar es Salaam.
“Nchi yetu itaadhimisha sherehe za kutimiza miaka 55 ya Uhuru wa
Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, 2016. Kitaifa, maadhimisho hayo
yatafanyika katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Mgeni rasmi katika
maadhimisho hayo atakuwa Dk John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania,” ilieleza taarifa iliyotolewa Jumatatu hii na
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi, Vijana
na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama.
Kwa mujibu wa Jenista, sherehe zinazotarajiwa kufanyika siku hiyo ya
kilele ya sherehe hizo ni gwaride la heshima lililoandaliwa na Vikosi
vya Ulinzi na Usalama, maonesho ya Kikosi cha Makomandoo pamoja na
gwaride la kimya kimya, burudani za vikundi vya ngoma za asili za mikoa
ya Mbeya, Pwani, Lindi na kimoja kutoka Zanzibar.
Aidha Jenista Muhagama alisema “Kwa niaba ya serikali, natoa mwito
kwa wananchi wote nchini kusherehekea siku hii kwa kuwakumbuka waasisi
wetu waliotetea na kutuletea Uhuru wa nchi yetu. Niwaombe Watanzania
wote katika kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru tuunge mkono juhudi za Rais
wetu Mheshimiwa Dk John Magufuli katika kuimarisha uchumi wa viwanda kwa
maendeleo ya nchi yetu.”
Kauli mbiu ya kutimiza miaka 55 ya Uhuru ni “Tuunge mkono jitihada
za kupinga rushwa na ufisadi na tuimarishe uchumi wa viwanda kwa
maendeleo yetu.”
0 maoni:
Post a Comment