Miaka 5 tangu kifo cha Kanumba: Bongo Movie inaendelea kusuasua

Moja kati ya tamaduni na desturi za Kiafrika ni kuamini katika wafu. Watu wa jamii nyingi za kiafrika wanaishi katika dunia hii. Inaaminika mtu akifa ana uwezo wa kukupa baraka na laana, hivyo si ajabu kuona makabila mbalimbali kwenda makaburini kupata baraka au kuondoa laana baada ya mambo kwenda ndivyo sivyo.
Alfajiri ya tarehe 7/04/2012 gwiji wa filamu za bongo movie marehemu Steven Kanumba aliaga dunia! Tarehe 07/04 atatimiza miaka mitano tangu apate pumziko lake la milele. Hakuna ambaye hajui achilia mbali kipaji chake maridhawa lakini juhudi na kujituma kwa icon huyu wa bongo movie. Alifanya kila aliloweza kuhakikisha tasnia ya filamu inafikia kule walipo wenzetu waliopiga hatua katika tasnia hiyo – Kanumba ameondoka na kafa na bongo movie!
Baada ya Kanumba kufariki, waliibuka watabiri mbalimbali waliotabiri kuwa hicho ndio kilikuwa kifo cha bongo movie. Pengine waliona mbele na wana kila sababu ya kuonekana ni watabiri haswa kwani lile walilotabiri ndiyo tunalishuhudia sasa!
Hakuna jipya linaloendelea kwa sasa kwenye kiwanda cha bongo movie. Kila kukicha image mbaya juu yao inaongezeka kuliko idadi ya scenes, skendo ndo zimezidi kuliko kazi wanazofanya. Kiukweli inahuzunisha na kusononesha sana.
Inahuzunisha hasa ukikumbuka kuwa pengine Uncle JJ angekuwepo tusingekua hapa. Wakati huu ambao idadi ya mitandao ya kijamii na watumiaji wake hapa nchini imekuwa kubwa, naamini hii ingekuwa fursa adhimu kwa Steven ambaye kila uchwao alikuwa akitafuta fursa ya kuhakikisha kazi zake zinapenya na kuwafikia watu wengi zaidi. Dada zangu na kaka zangu wa bongo movie wao wanaitumia mitandao hiyo kuonyesha mavazi na mali wanazomiliki, kutupa na kujibu madongo na siku hizi kuweka matangazo uchwara!
Kwa wote mnaohusika kwenye kiwanda bongo movie, sasa mna kila sababu ya kujisikia aibu kwa watu kumkumbuka marehemu eti kwa kitu ambacho mngeweza kufanya tena pengine kwa ufanisi mkubwa kulinganisha na yeye. Lakini badala yake nyie kwa nyie mnachukiana, mnaoneana wivu usio na maana na mmejaa majungu(hii ni kwa mujibu wenu wenyewe mmesikika mkisema) au mnasubiri siku ya kuadhimisha kifo chake mkatambike?
Kila nikiangalia naona kuna fursa kwa nyie kuamka tena na kuliteka soko la ndani na Afrika kwa ujumla, mna haiba, mvuto, vipaji vya kuweza kufanya hivyo. Najua na natambua changamoto mnayoipata katika wizi wa kazi na maslahi mnayopata lakini hamuwezi kukaa tu mkilalamika pasi kuungana. Kuweni wabunifu katika kazi zenu, mkianza kuwekeza nguvu katika kufanya yaliyo bora ni rahisi kutatua changamoto mlizonazo.
Brothers and sisters LuLu, Wema, Kajala, Uwoya, JB, Gabo, Richie na wengine, msione kawaida kuona mitaani kazi za Kihindi na Kinijeria zilizotafsiriwa zikitazamwa kwa wingi kuliko movies za kitanzania. Wabongo wanapenda kazi zenu wanaangalia hizi kwa kuwa sokoni hakuna kazi zenu na zilizopo hazina ubora wa hadithi, picha, sauti na uigizaji pia.
Mwaka huu uwe wa mabadiliko kwenu, oneni wivu kuona nyie ndo mnafanya kazi ya kupromote kazi za Bongo Flava na Bongo Flava hawana cha kusapoti kutoka kwenu. 2017 uwe mwaka wa mabadiliko kwenu na tuone mkiliteka soko kwa mara nyingine.

0 maoni:

Post a Comment